1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Iran kutoridhishwa na maelezo ya Rouhani

Yusra Buwayhid
28 Agosti 2018

Bunge la Iran limeukataa utetezi wa Rais Hassan Rouhani walipomtaka ajieleze juu ya kuporomoka kwa uchumi na kupanda kwa gharama za maisha na limemtaka ajieleze mbele ya mahakama.

https://p.dw.com/p/33sCq
Iran Präsident Hassan Rohani
Picha: irna

Rouhani amekiambia kikao cha bunge leo kwamba Iran itapambana na vikwazo ilivyowekewa tena na Marekani na kuapa kwamba serikali yake itaishinda njama yoyote iliyopangwa na nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Bunge la Iran limemwita Rouhani kwa mara ya kwanza tokea alipoingia madarakani 2013, kujibu maswali juu ya udhaifu wa uchumi na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, lakini kiongozi huyo alisema matatizo yote yalianza pale Marekani ilipoiwekea tena vikwazo Iran.

Akizungumza mbele ya bunge katika hotuba iliyorushwa mubashara katika kituo cha televisheni ya taifa, Rouhani amesema serikali yake itapambana na Marekani.

"Hatutaruhusu kikundi cha wapinzani wa Iran ambacho leo kimekusanyika katika Ikulu ya Marekani kupanga njama dhidi yetu. White House haitakuwa na furaha kitakapomalizika kikao cha leo," amesema Hassan Rouhani.

Iran Wirtschaftsminister Massud Karbassian Amtsenthebung
Kikao cha bunge la IranPicha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Wabunge kutoridhishwa na maelezo ya Rouhani

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, bunge lilipiga kura ya kutokuridhika na utetezi wa rais huyo mwenye msimamo wa wastani, wakisema kuwa katika masuala matano waliyomuuliza ni moja tu ndilo alilowatosheleza kwa maelezo.

Tayari wabunge walishawapigia kura ya kutokuwa na imani nao mawaziri wawili wa serikali ya Rouhani mwezi huu. Kwa mujibu wa kanuni za kibunge nchini Iran, endapo wabunge hawakuridhishwa na majibu ya ofisi ya rais kwenye masuala muhimu ya nchi, masuala hayo hupaswa kupelekwa mbele ya muhimili wa mahakama kwa uhakiki.

Rouhani anashinikizwa na wanasiasa wa misimamo mikali na hata kutoka katika kambi yake ya wanamageuzi, wanaomtaka afanye mabadiliko ya baraza la mawaziri kutokana na kuanguka kwa uchumi, baada ya uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Ingawa matatizo ya kiuchumi yana umuhimu, Rouhani amesema muhimu zaidi ni kwamba watu wamepoteza imani juu ya maslahi ya Jamhuri hiyo ya Kiislam na wana shaka na nguvu ya uongozi wake.

Rouhani ambaye alipunguza mvutano na nchi za Magharibi baada ya kusaini makubaliano ya kinyuklia na nchi zenye nguvu duniani 2015, hivi sasa anakabiliana na upinzani kutoka kwa wanasiasa wenye misimamo mikali nchini humo kutokana na Marekani kuamua kujiondoa katika makubaliano hayo.

Rais huyo wa Iran imewaambia wabunge hao kwamba kuna njia nyengine ya tatu ya kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi mbali na kubaki au kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia. Hakufafanua zaidi kuhusu njia hiyo, lakini amesema ameijadili pamoja na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, jana Jumatatu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap

Mhariri: Mohammed Khelef