1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa Tanzania waandamana kulaani mauaji ya Mwandosi

11 Septemba 2012

Waandishi wa habari nchini Tanzania wameanzisha maandamano kulaani mauwaji ya mwandishi mwenzao, Daudi Mwangosi, ambaye aliuwawa hivi karibuni wakati akiwa kazini wilayani Mufindi mkoani Iringa.

https://p.dw.com/p/166d0
Polisi wa kutuliza fujo nchini Tanzania.
Polisi wa kutuliza fujo nchini Tanzania.Picha: AP

Wakiwa na nyuso za huzuni huku wakivalia nguo nyeusi na kubeba mabango kadhaa, waandishi wa habari wamejitokeza mitaani kupinga na kulaani vikali tukio la mauwaji ya mwandishu huyo wa habari, ambalo ni la kwanza la aina yake kutokea nchini Tanzania.

Mikoa kadhaa imeripotiwa kufanikisha maandamano hayo, ikiwemo mkoani Iringa ambako Daudi aliuwawa na ndiko pia alikokuwa akiendesha shughuli zake za uandishi wa habari.

Pamoja na mvua za rasha rasha zilizonyesha nyakati za asubuhi jijini Dar es Salaam, hali hiyo haikuwazuia waandishi habari kujitokeza kwa wingi wakianzisha maandamano kutoka zilipo ofisi za kituo cha televisheni Channel Ten ambako Daudi akifanyia kazi mpaka viwanja vya Jangwani vilivyoko pembezoni kidogo ya katikati ya jiji.

Kwenye kilele cha maandamano hayo kumetolewa matamko ya kulaani mauwaji hayo, huku mengine yakikosoa mwenendo wa vyombo vya dola. Miongoni mwa waliotoa matamko hayo ni mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Jackton Manyerere, na mhariri wa siku nyingi nchini humo, Jesse Kwayu.

Polisi wa Tanzania wakiingia mitaani kukabiliana na waandamanaji.
Polisi wa Tanzania wakiingia mitaani kukabiliana na waandamanaji.Picha: AP

Katika hali ya kushangaza,waziri wa mambo ya ndani Emmanuel Nchimbi alijipenyeza kwenye kusanyiko hilo na baadaye kutoa maelezo kadhaa, lakini alishindwa kuendelea kutokana na mayowe yaliyomtaka aondoke kwenye eneo hilo.

Kundi moja la waandishi wa habari limesema linatazamia kuchukua hatua za kisheria kuwabana askari wote waliohusika kwenye mauwaji hao.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef