1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Vyama vya kisiasa Pakistan vyaunda serikali ya muungano

14 Februari 2024

Vyama viwili vikuu vya kisiasa Pakistan vilivyoungana kumuondoa Imran Khan kama Waziri Mkuu mwaka 2022 vimesema vitaunda serikali ya mseto kuiongoza nchi hiyo baada ya uchaguzi kushindwa kumpata mshindi wa moja kwa moja.

https://p.dw.com/p/4cNsc
Pakistan, Lahore | Shehbaz Sharif
Vyama vya kisiasa nchini Paistan vyakubaliana kuunda serikali ya muunganoPicha: K.M. Chaudary/AP/picture alliance

Chama cha Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif na washirika wake walitangaza jana jioni kwamba kwa pamoja wataunda serikali ya muungamo na kumaliza mvurugano uliokuwepo tangu wiki iliyopita ambako hakuna hata chama kimoja kilichoshinda wingi wa kura katika uchaguzi wa bunge. Kiongozi wa chama cha Pakistan People's Party cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Asif Ali Zardari, alitangaza muungano huo na kusema wako tayari kupambana na matatizo ya Pakistan.

"Tumeamua tutaungda serikali ya pamoja, Mungu akipenda tutaiondoa Pakistan kutoka katika mambomengi magumu, na mungu akipenda pia kila tatizo tunalokupambana nalo Pakistan aidha kiuchumi au tatizo la kigaidi au maridhiano, tutapatana na tutaleta vyama vyote pamoja kikiwemo chama cha PTI ," alisema Zardari.

Uamuzi huu umekuja saa kadhaa baada ya vyama hivyo ambayo yvote ni wapinzani wa waziri mkuu wa zamani aliyefungwa jela kwa makosa ya ufisadi Imran Khan, kukutana mjini Islamabad.

Vyama vya kisiasa Pakistan vyaanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto

Mkutano huo ulihudhuriwa na  kiongozi huyo wa chama cha Pakistan People's Party (PPP) Asif Ali Zardari, na chama cha Nawaz Sharif cha Pakistan Muslim League PML-N akiwemo kakaake mdogo Shehbaz Sharif, aliyechukua nafasi ya Imran Khan alipoondolewa katika uwaziri mkuu mwaka 2022 kupitia kura ya kutokuwa na imani nae.

Nawaz Sharif huenda akavikwa taji la uwaziri Mkuu mpya wa Pakistan

Pakistan Lahore | Ehemaliger Premierminister Pakistans Nawaz Sharif
Waziri Mkuu wa Zamani wa Pakistan anaetarajiwa kuiongoza tena nchi hiyo, Nawaz SharifPicha: Ali Kaifee/DW

Katika mkutano huo Shebaz hakusema ni nani atakaekuwa chaguo lao, kuchukua nafasi ya Waziri Mkuu lakini inaaminika kuwa Nawaz Sharif  wa chama cha (PML-N)  kinachoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo huenda akaiongoza serikali hiyo mpya. Shehbaz aliyekuwa waziri mkuu katika serikali iliyopita, kabla ya bunge kuvunjwa alisema angelipenda kumuona kaka yake mkubwa ambaye amewahi kuiongoza nchi hiyo mara tatu kurejea tena uongozini.

Chama cha Muslim League kimekuwa katika mazungumzo na Zardari na washirika wengine baada ya uchaguzi wa bunge. Wagombea walioungwa mkono na chama cha Imran Khan cha Tehreek-e-Insaf kilishinda viti 93 kati ya 265 vilivyopo na idadi hiyo haikuwa inatosha kwa chama hicho kuunda serikali. Chama cha Nawaz Shariff kilipata viti 75 huku chama cha Zardari kikishinda viti 54 bungeni.

Wanasiasa waombwa kuwa watulivu na wakomavu wa kisiasa Pakistan

Uamuzi wa vyama vya Sharif na Zardari kuunda serikali ya pamoja umekuja baada ya chama cha Khan kukataa kuingia katika mazungumzo na vyama hivyo viwili, maana baada ya kuhsinda viti vingi bungeni na kutokuwa bado na nafasi ya kuunda serikali pekee kilitakiwa kuungana na cha kingine kuunda serikali lakini chama hicho kikakataa kuchukua hatua hiyo. Vyama hivyo vilivyoungana vilisema hata hivyo viko tayari kuzungumza na Khan aliyeko jela ili kukijumuisha pia chama cha PTI katika serikali ijayo.

Kulingana na katiba ya Pakistan, rais Arif Alvi atafungua kikao cha bunge Februari 29 ili wabunge waliochaguliwa waweze kuapishwa kisha baadae bunge litamchagua waziri mkuu mpya.

ap/afp/ reuters