1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuguvugu la vizibao vya njano latimiza mwaka mmoja

Daniel Gakuba
16 Novemba 2019

Polisi wa Ufaransa wametumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa vuguvugu la vizibao vya njano waliokuwa wakisherehekea mwaka mmoja tangu kuanza maandamano ya kupinga sera wanazosema zinawapendelea matajiri.

https://p.dw.com/p/3TA4q
Frankreich | Demonstrationen anlässlich des 1. Jahrestages der Gelbwestenproteste
Picha: Reuters/C. Platiau

 Usalama umeimarishwa katika mitaa ya jiji la Paris, na hadi alasiri Jumamosi, watu 46 walikuwa wamekamatwa. Waandamanaji wa vuguvugu la Vizibao vya Njano walikuwa wakifanya fujo, baadhi wakijaribu kuvunja vioo vya madirisha ya maduka ya jumla. Wengine walionekana wakiwarushia mawe maafisa wa usalama, na kuwasha mioto wakitumia taka na matairi ya pikipiki. Uwanja cha Place d'Italie ulioko kusini-mashariki mwa Paris ulishuhudia makabiliano makubwa.

Mapema asubuhi Jumamosi waandamanaji hao walivunja madirisha ya jengo la benki na kuhujumu kituo cha kuegesha mabasi, kabla ya polisi kuwasili na kuwatawanya. Polisi hao walifanikiwa kudhibiti hali ya mambo. Matukio kama hayo yalishuhudiwa pia katika miji mingine nchini kote Ufaransa.

Wanaharakati watoka huku na huko kuja Paris

Corentin Pihel mwenye umri wa miaka 28 ambaye alisafiri kutoka Montpellier hadi Paris kushiriki katika maadhimisho hayo, amesema vuguvugu la vizibao vya njano limekuwa chombo cha mshikamano wa wanyonge.

Frankreich | Demonstrationen anlässlich des 1. Jahrestages der Gelbwestenproteste
Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanajiPicha: Reuters/C. Platiau

''Mwanzoni vuguvugu hili lilinivuia kwa namna lilivyohamasisha watu wa mashinani na kuunda sauti kubwa ya wanunuzi'', alisema Pihel na kuongeza kuwa kadri vuguvu hilo lilivyozidi kupanuka, limekuwa mshikamano wa watu wanaotaka kuwa na kauli juu ya namna maisha yao yanavyopaswa kuendeshwa.

Mwandamanaji mwingine, Cathy Nauleau aliyefika Paris kutoka mashariki mwa Ufaransa, amesema ingawa bado vuguvugu lao halijapa mafanikio makubwa, ''hatutakata tamaa''.

Vuguvugu la vizibao vya njano lilianza mwezi Novemba 2018 kama upinzani dhidi ya azma ya serikali ya kuanzisha kodi mpya kwa mafuta ya dizeli, yakienea katika maeneo yote ya nchi na kusimamisha kabisa shughuli za biashara. Jina la vuguvugu hilo liliokana na vizibao ambavyo kisheria mtu yeyote mwenye kuendesha gari nchini Ufaransa anapaswa kuwa nacho ndani ya gari lake.

Serikali yaridhia matakwa yao

Frankreich | Demonstrationen anlässlich des 1. Jahrestages der Gelbwestenproteste
Waandamanaji walitoka kona zote za Ufaransa kushiriki maadhimisho mjini ParisPicha: Reuters/C. Platiau

Chini ya shinikizo la vuguvugu hili, serikali ya Rais Macron aliiondoa kodi hiyo iliyopigiwa kele, na imetangaa nafuu ya kodi kwa familia ambayo itaaanzishwa mwaka ujao wa 2020, ikiwa na thamani ya yuro bilioni 9.8.

Mjini Paris, mamia ya waandamanaji walipeperusha bendera ya taifa ya Ufaransa, wakipiga ngoma na kupuliza vipenga, na kuimba wimbo ambao umekuwa nembo ya vuguvugu lao, unaosema, ''Tuko hapa, hata kama Rais Emmanuel Macron hatutaki.''

Polisi waliojihami kwa silaha na zana nyingine za kuzima fujo walipiga doria kwenye mnara wa Arc de Triomphe mkabala na mtaa maarufu wa Champs-Elysees, ambao mwaka jana ulikuwa shabaha ya ya waandamanaji.

Watu wenye dukuduku kama la wanaharakati wa vuguvugu la vizibao vya njano katika nchi nyingine za Ulaya, walilivaa vazi hilo kama ishara ya hasira zao dhidi ya sera za serikali wasizozipenda.

ape, rtre