1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya Ebola vyazua hali ya taharuki Ulimwenguni

31 Julai 2014

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ameagiza kufungwa kwa shule zote nchini humo na kuwataka wafanyakazi wa umma wasio na majukumu ya kimsingi kwenda likizoni kama sehemu ya kujaribu kupunguza kusambaa kwa Ebola

https://p.dw.com/p/1Cmj3
Picha: Reuters

Katika hotuba kwa taifa jana jioni, Rais Johnson Sirleaf amesema serikali yake imetoa kiasi cha dola milioni tano kutekeleza mpango makhususi wa kukabiliana na virusi hivyo hatari vya Ebola ambavyo vimesababisha vifo vya kiasi ya watu 130 nchini Liberia pekee.

Kiasi ya watu 670 wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea,Liberia,Sierra Leone tangu kuzuka kwa Ebola mwezi Februari mwaka huu huku kiasi ya visa 1,200 vya maambukizi vikiripotiwa.

Sirleaf ametangaza kesho Ijumma kuwa siku ya mapumziko katika taasisi zote za umma ili kuruhusu kufanyika kwa zoezi la kupiga dawa za kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo.

Sierra Leone pia yachukua tahadhari

Wafanyakazi wa umma ambao huduma zao hazihitajiki kwa dharura watatakiwa kuwa katika kipindi cha mapumziko ya lazima kwa siku thelathini zijazo na masoko yote yaliyoko katika maeneo ya mipakani pia kufungwa.

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf
Rais wa Liberia Ellen Johnson SirleafPicha: Getty Images

Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma ametangaza leo kuwa watu hawatarusiwa kuingia au kutoka maeneo yaliyoathirika nchini humo na maafisa wa usalama watatumika kulitekeleza hilo.

Rais Koroma pia ametangaza amefutilia mbali ziara ya kuelekea mjini Washinton kuhudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Afrika na wa Marekani kushughulikia tatizo hilo la Ebola nchini mwake.

Kusambaa kwa ugonjwa huo umeziweka nchi nyingi ulimwenguni katika hali ya tahadhari kuzuia kufika nchini mwao huku shirika la madaktari wasio na mipaka MSF likionya kuwa mkurupuko huo umeshindikana kudhibitiwa kwa sasa.

Nchi za magharibi zafuatilia hali

Shirika la amani la kutoa misaada la Marekani limetangaza linawahamisha wafanyakazi wake kutoka nchi hizo za magharibi zilizoathirika kutokana na kuzuka na kusambaa kwa Ebola.

Maafisa wa afya wanaokabilaiana na Ebola
Maafisa wa afya wanaokabilaiana na EbolaPicha: picture-alliance/dpa

Na huko Uingereza,kamati ndogo ya bunge inayoshughulikia majanga ilifanya kikao cha dharura hapo jana kilichoongozwa na waziri wa mambo ya nje Philiph Hammond ambaye alisema licha ya kuwa hakuna kisa chochote cha Ebola ambacho kimeripotiwa nchini humo,ni muhimu kuchukua hatua za tahadhari ya mapema ili kutathmini hali ilivyo na kujiandaa kwa uwezekano wowote.

Umoja wa Ulaya umesema umejiandaa vilivyo kuwatibu waathiriwa wa Ebola iwapo utazuka katika nchi yoyote mwanachama ikizingatiwa kuwa ni vigumu kubashiri iwapo utafika Ulaya au la kutokana safari za raia wake kutoka nchi za kigeni.

Virusi vya Ebola vinaweza kumuua muathiriwa katika kipindi kifupi sana cha siku chache tu baada ya kuambukizwa. Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni kuwa na homa kali,maumivu ya viungo,kutapika na kuharisha.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/Reuters/Afp

Mhariri: Iddi Ssessanga