Viongozi wa zamani wa Nigeria wamtaka Rais Yar'Adua kukabidhi madaraka kwa makamu wake.
29 Januari 2010Kundi la viongozi wa zamani wa Nigeria wamemtaka Rais wa nchi hiyo, Umaru Yar'Adua, ambaye anaugua kuchukua hatua madhubuti na kumkabidhi madaraka makamu wake kwa ajili ya kukaimu nafasi yake. Wito huo umetolewa jana Alhamisi katika barua iliyosainiwa na aliyekuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Yakubu Gowon, kwa niaba ya viongozi hao.
Viongozi wengine waliowasilisha wito huo kwa Makamu wa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, mjini Abuja, na wakuu wa mabaraza mawili ya bunge, ni Shehu Shangari na Ernest Shonekan. Wengine ni aliyewahi kuwa makamu wa rais, Alex Ekwueme, wanasheria wakuu wa zamani, Mohammed Uwais, Alfa Belgore na Idris Kutigi, pamoja na mkuu wa zamani wa majeshi, Jenerali Theophilus Danjuma. Viongozi hao wa zamani wamesema kuwa ni muhimu kulitatua suala hilo kwa haraka kwa kutoa waraka rasmi utakaomuwezesha makamu wa rais wa nchi hiyo kukaimu madaraka. Wamesema wameandika barua hiyo kufuatia umuhimu wa mapitio jumla ya hali ya kisiasa ya nchi hiyo katika kipindi cha hivi karibuni, lakini zaidi hasa ni kufuatia kuugua kwa rais na kutokuwepo kwake madarakani kwa muda mrefu.
Shinikizo kwa Rais Yar'Adua kujiuzulu
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na shinikizo la kumtaka Rais Yar'Adua kuachia madaraka. Hata mshauri wake mwenyewe na mtangulizi wake, Olusegun Obasanjo, ametoa wito kwa kiongozi huyo kujiuzulu. Baada ya kikao chao cha siku mbili, baraza la seneti lilimtaka Rais Yar'Adua kuliarifu rasmi bunge kuhusu likizo yake ya matibabu, kulingana na sheria husika ya kusafisha njia kwa naibu wake kukaimu nafasi yake. Hata hivyo, saa chache baadaye, baada ya kutolewa azimio hilo la wabunge, baraza la mawaziri liliamua kuwa Rais Yar'Adua anaweza kuendelea na kazi zake za ofisini na kwamba kuwa katika eneo la mbali kwa ajili ya matibabu hakutamfanya rais huyo kutotekeleza utendaji wake wa kazi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amesema Rais Yar'Adua mwenye umri wa miaka 58 ambaye yuko nchini Saudi Arabia kwa matibabu ya moyo kwa zaidi ya miezi miwili sasa, atarejea nchini kwake hivi karibuni. Katika hafla ya kupokea hati za utambulisho wa mabalozi wanne wapya, Jonathan aliwashukuru kwa hatua yao ya kujali hali ya kiafya ya Rais Yar'Adua na kuwahakikishia kwamba kiongozi huyo atarejea nchini kwake hivi karibuni.
Jumuiya ya kimataifa
Katika hatua nyingine, mataifa yenye nguvu duniani jana Alhamisi yamekemea vikali mzozo uliopo kwa sasa juu ya afya ya rais wa Nigeria na kulaumu kauli zisizokuwa za uhakika ambazo zinasababishwa na kutokuwepo kwake, wakati makamu wake aliahidi kwamba angeweza kurejea nyumbani mapema. Taarifa ya pamoja ya Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza na Ufaransa imeeleza kuwa Nigeria iko katika wakati usio na uhakika kwa sababu ya ugonjwa wa muda mrefu wa Rais Yar'Adua. Mataifa hayo yalisema yanapongeza jitihada za kikatiba nchini Nigeria, taifa lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika na moja kati ya yale yenye kutoa mafuta kwa wingi, kwa kutatua suala la mamlaka zinazoiongoza nchi hiyo kufuatia kutokuwepo madarakani kwa muda mrefu Rais Yar'Adua.
Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Miraji Othman