1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTunisia

Viongozi wa upinzani wakamatwa Tunisia

18 Aprili 2023

Polisi wa Tunisia wamewakamata maafisa watatu mashuhuri wa chama kikuu cha upinzani cha Ennahda, saa chache baada ya kumkata kiongozi wa chama Rached Ghannouchi, mkosoaji mashuhuri wa Rais Kais Saied.

https://p.dw.com/p/4QEL2
Tunesien Tunis | Rached Ghannouchi
Rached GhannouchiPicha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Afisa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ameliambia shirika la habari la serikali, TAP kwamba Ghannouchi alikamatwa jana Jumatatu kwa madai ya uchochezi.

Shirika hilo limeripoti kwamba maafisa wa usalama walipekua nyumba yake na kupata ushahidi unaoweza kutumika katika uchunguzi dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani, kabla ya kumpeleka katika kile ambacho chama chake kimesema ni mahala pasipojulikana.

Kupitia ukurasa rasmi wa Facebook chama hicho cha Ennahda kimetoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Ghannouchi na kuitaja hatua ya kukamatwa kwake kuwa mwanzo wa uwezekano wa kutaka kukipiga marufuku chama hicho cha Kiislamu.

Huku haya yakijiri idara ya mahakama inawachunguza maafisa wengine wawili wa chama cha  Ennahda, Ali Laaraydh waziri mkuu wa zamani, na Noureddine Biri, waziri wa zamani wa sheria, ambao wako gerezani, katika kesi inayohusiana na ugaidi na uchochezi dhidi ya taasisi za serikali.

Mashataka ya waliokamatwa

Tunesien Tunis | Proteste | Rached Ghannouchi
Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Upinzani unasema mashtaka hayo ni ya uzushi na ya yamechochewa kisiasa , na kumshutumu Rais Kais Saied kwa kudhoofisha misingi ya demokrasia na kuweka mfumo wa kanuni za utawala wa mtu mmoja.

Akizungumza baada ya kukamatwa kwa Ghannouchi Afisa mwandamizi wa chama cha Ennahda Ridha Chaibi amesema

"Kukamatwa kwa Rached Ghannouchi leo ni kuimarika kwa sera ya unyanyasaji na kuwalenga wapinzani wa kisiasa, na hii ni moja ya hatua nyingi zilizotangulia - ikiwa ni pamoja na kuwalenga wanaharakati na wanasiasa. Sasa makumi yao wamekamatwa na wako gerezani wakisubiri kesi zisizojulikana, tuhuma zisizo na uthibitisho, na ukweli ambao hakuna anayejua. Sheria ya ugaidi ambayo kimsingi inatumika kwa magaidi inatumiwa na Kais Saied na mamlaka yake kwa wanasiasa katika ukiukaji wa wazi wa haki zao kama wafungwa wa kisiasa."

Madaraka ya rais Kais

Tunesien I Protest gegen Kais Saed in Tunis
Picha: Yassine Mahjoub/NurPhoto/picture alliance

Tangu 2021, Saied amezidisha mamlaka yake kwa kuvunja bunge, na kuitisha uchaguzi wa mapema. Hatua zilizopelekea kudhoofika kwa uwakilishi.Rais Kais pia alifanya kura ya maoni ya katiba, ambayo ilimpa mamlaka makubwa zaidi.

Tunisia, iliyoonekana kwa muda mrefu kama mfano wa pekee wa mafanikio ya demokrasia baada ya vuguvugu la kiarabu mnamo mwaka 2010 hadi 2011 lakini  bado inakabiliwa na misukosuko ya kiuchumi na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira.

 

/Reuters,dpa