Hakuna maamuzi katika suala la wakimbizi Ujerumani
1 Novemba 2015Ujerumani taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya na kivutio kikuu cha wahamiaji inatarajia watafuta hifadhi kati ya 800,000 na milioni moja kuwasili mwaka huu idadi hiyo ikiwa ni maradufu kulinganishwa na mwaka jana na ni kubwa kabisa kulinganishwa na nchi nyengine yoyote ile ya Umoja wa Ulaya iliopokea wahamiaji.
Mmiminiko huo wa wahamiaji nchini umesababisha mgawanyiko ndani ya serikali ya mseto ambapo chama ndugu cha jimbo la Bavaria CSU katika muungano wa kihafidhina na chama cha Merkel CDU kinadai kuchukuliwa kwa hatua kali kukabiliana na hali hiyo wakati chama chengine cha tatu katika serikali ya mseto SPD kikipinga.
Msemaji wa serikali Steffen Seibert ameyaelezea mazungumzo hayo yaliofanyika Jumapili kati ya viongozi watatu wa vyama hivyo kuwa ya "tija" lakini amesema viongozi hao watakutana tena Alhamisi.
Seibert amesema "wamekuwa na msimamo wa pamoja kwa mambo mengi lakini kuna baadhi ya vipengele ambavyo bado viko wazi na inabidi waafikiane." Ameongeza kusema kwamba vipengele hivyo ni pamoja na wazo la kuanzisha kile kinachoitwa "kanda za kujishikiza kwa muda wahamiaji katika maeneo ya mipakani " wakati maombi yao ya kutafuta hifadhi yakishughulikiwa.
Kishindo cha Bavaria
Kiongozi wa SPD Sigmar Gabriel ameondoka katika ofisi ya kansela akiwa hana furaha baada ya mkutano wake wa masaa mawili na Kansela Angela Merkel na Horst Seehofer kiongozi wa chama cha CSU cha Bavaria.
Jimbo la Bavaria ndio lenye kubeba mzigo mkubwa wa wimbi hilo la wahamiaji wanaowasili nchini na Seehofer yuko kwenye shinikizo kubwa kutoka serikali za mitaa za jimbo lake kuishinikiza serikali kuu ya Ujerumani kudhibiti wimbi hilo la wahamiaji wanaowasili kutoka kwenye nchi za kimaskini zilizokumbwa na mizozo za Mashariki ya Kati,Asia na Afrika.
Katika wiki za hivi karibuni alikuwa ametowa vitisho kadhaa kwa Merkel ikiwa ni pamoja na kuiburuza serikali mahakamani kutokana na sera zake za wahamiaji na kuja kuachana na tishio hilo dakika za mwisho. Baadhi ya wanachama wa chama chake cha CSU wanataka kuimaraishwa kwa ulinzi wa mipakani au hata kufungwa kwa mipaka hiyo.
Umashuhuri washuka
Ili kuzima mivutano hiyo wahafidhina walitarajia Seehofer atatoka katika mkutano huo akiwa na makubaliano juu ya vituo hivyo vya kujishikiza wahamiaji katika maeneo ya mipaka.
Hata hivyo baadhi ya wanachama wa SPD walisema wasingekubali kuwepo kwa vituo hivyo na kwamba wahafidhina inabidi wakane kwamba vituo hivyo havitofanana na makambi ya mateso.
Mabishano kati ya washirika wa kihafidhina CDU na CSU yameathiri msimani wao kwa jamii.Uchunguzi wa maoni wa kila wiki uliofanywa na shirika la kufuatilia maoni ya wananchi la Emnid yameonyesha ushirika wa vyama hivyo unaungwa mkono kwa asilimia 36 ikilinganishwa na 43 hapo mwezi wa Augusti.
Chama cha SPD cha Gabriel kimepoteza asilimia moja kwa kuungwa mkono kwa asilimia 25. Chama cha mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani kimejiongezea asilimia moja na kufikia asilimia nane ya kuungwa mkono.
Gabriel mwezi uliopita alionya kwamba lazima wawashinde wale wenye mashaka na wakimbizi venginevyo watakuwa "wanapandikiza mabomu ya kijamii katika taifa lao" wakati mkuu wa jeshi la polisi nchini amesema mmiminiko wa wakimbizi usiokuwa na udhibiti unatowa tishio la usalama wa ndani.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri : Bruce Amani