Viongozi EU waidhinisha mazungumzo ya maandalizi Brexit
20 Oktoba 2017Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk alisema katika ujumbe wa Twita kuwa viongozi 27 wa kanda hiyo waliokutana mjini Brussels walikubaliana kuanzisha maadalizi ya mazungumzo ya biashara, baada ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel kusema hapo awali kwamba licha ya ucheleweshaji katika mazungumzo, kuna matumaini ya kufanikisha makubaliano ya mwisho.
Taarifa ya maandishi ilioidhinishwa na viongozi hao ilisema Umoja wa Ulaya utachelewesha uamuzi juu ya kuanzisha hatua nyingine ya mazungumzo hadi mkutano ujao wa kilele mwezi Desemba, lakini walikubaliana kuanzisha majadiliano ya ndani ya maandalizi kuhusu biashara na uwezekano wa makubaliano ya mpito.
Kasi ndogo ya mazungumzo, hasa kuhusu wajibu wa kifedha wa Uingereza, ilichochea hofu kwamba nchi hiyo inaweza kuondoka Umoja wa Ulaya Machi 2019 bila makubaliano, na hivyo kuweka hatari ya sokomoko la kisheria na kiuchumi.
Merkel, kiongozi mwenye nguvu zaidi katika Umoja wa Ulaya, amesisitiza kuwa hakutaka hilo litokee, na kuogeza kuwa anachotaka ni makubaliano ya wazi na siyo tu suluhu isioyatabirika, akisisitiza lakini, kwamba Uingereza laazima itimize wajibu wake wa kifedha.
"Tunatumai kwamba kufikia Desemba tutakuwa tumepiga hatua za kutosha kuwezesha awamu ya pili kuanza lakini hiyo inategemea umbali gani Uingereza itakuwa imefikia ili tuweze kusema kwamba inatosheleza juu ya masuala makuu ya awamu ya kwanza," alisema Merkel na kuongeza kuwa, katika hayo suala la malipo ya fedha ndiyo muhimu zaidi.
'Hakuna muuzija'
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May aliungana na wenzake 27 kwa kifungua kinywa cha kikazi kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya, kabla ya kuondoka kuwapa nafasi ya kuzungumzia hali ya mazunguzo ya Brexit.
Umoja wa Ulaya unakubaliana kwamba kati ya masuala matatu makuu ya kutengana, suala la haki za raia ndiyo limepiga hatua lakini masuala yanayozusha ubishani zaidi yanaendelea kuwa malipo ya fedha za kujiondoa na mpaka wa Ireland ya Kaskazini na Ireland.
Rais wa Halmashuauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, ambaye hapo awali alisema itakuwa muujiza kuendeleza mazungumzo hayo katika mkutano wa sasa, alisema Ijumaa kuwa haamini kwamba kutakuwepo na muujiza.
Duru kutoka Umoja wa Ulaya imesema kuanza kwa maandalizi kuhusu miongozo ya mazungumzo ya biashara kutaokoa muda ikiwa uamuzi wa kisiasa utachukuliwa kusonga mbele mwezi Desemba.
Uhusiano kati ya EU na Uturuki
Mkutano huo pia ulijadili juu ya uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, ambapo viongozi wameiomba Halmashauri kuu kuzingatia njia ya kupunguza au kuhamisha fedha za ufadhili zilizopangiwa kutolewa kwa Uturuki kama sehemu ya maombi yake ya kuwa mwanachama wa umoja huo.
Umoja wa Ulaya uliahidi kuilipa Uturuki kiasi cha euro bilioni 4.45 kati ya mwaka 2014 na 2020 kama sehemu ya majadiliano ya kujiunga na umoja huo. fedha hizo zinalenga kuisaidia Uturuki kuboresha utawala wa sheria kulingana na vigezo vya umoja huo.
Mazungumzo juu ya kujiunga kwa Uturuki na Umoja wa Ulaya pamoja na kupanua umoja wa forodha kati ya EU na Uturuki yamekwama mnamo wakati uhusiano wa kidiplomasia unazidi kuwa baridi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre,ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman