1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi Afrika watakiwa kufanya siasa safi

Hawa Bihoga, Dar es salaam31 Julai 2019

Kitabu chenye anwani 'Misingi 15 ya Amani' ambacho kimezinduliwa Tanzania, kimeangazia namna ya ufanywaji wa siasa safi kunavyoweza kuliweka bara la Afrika katika hali ya utulivu na amani.

https://p.dw.com/p/3N6KJ
Konferenz in Kampala
Picha: AP

Viongozi wa bara la Afrika wametakiwa kufanya siasa safi na kuheshimu imani za watu kwa misingi ya kutengeneza mataifa yenye amani na mshikamo kwa lengo la kuwa na dunia ilio salama.

Hayo yamesemwa katika uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na mwanazuoni wa Kiislamu kikiwa na jina ya Misingi 15 ya amani ambapo mbali na mambo mengine, kimeangazia namna ya ufanywaji wa siasa safi kunavyoweza kuliweka bara la Afrika katika hali ya utulivu na amani huku likiwa huru dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo vita, migogoro ya kisiasa, kudorora kwa uchumi pamoja na njaa.

Mwandishi wa kitabu hicho kilichosheheni kurasa mia moja kumi na tatu shekhe Mohammed Iddi ameiambia hadhira kuwa wanasiasa wamekuwa na mchango mkubwa katika kuvuruga amani kwa kupenda kung'ang'ania mamlakani lakini waliopo nje ya mamlaka hutumia mbinu zinazohatarisha amani katika kuyataka madaraka.

Rais wa zamani wa Tanzania Alhaji Hassan Mwinyi ni miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi wa kitabu hicho kinachohimiza amani.
Rais wa zamani wa Tanzania Alhaji Hassan Mwinyi ni miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi wa kitabu hicho kinachohimiza amani.Picha: DW/E. Lubega

Aliongeza baadhi ya maneno yanayopatikana katika kitabu hicho kuwa kuna baadhi ya wanasiasa katika chama tawala wanaamini kila kinachotamkwa na upinzani kina mrengo wa chuki ama uchochezi, huku akinyooshea kidole chama tawala kinapaswa kiwe kioo cha uongozi bora kwani serikali ni zao la chama tawala na chama sio zao la serikali.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na rais wa awamu ya pili Wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Alhaji Hassan Mwinyi, alisisitiza haki na usawa kwa kila mmoja ili kuepuka migogoro ndani ya mataifa yanayosababisha watu kuyakimbia makazi yao na kuliacha taifa lao katika hali mbaya kiuchumi na miundo mbinu.

Misingi mingine iliotajwa katika kitabu hicho ni pamoja na umakini wa vyombo vya habari, kuvumiliana katika itikadi za kidini, uadilifu katika vyombo vya sheria, kuepuka aina zote za ubaguzi, kutopuuza makundi ya vijana pamoja na kuitafutia suluhisho mbadala migogoro ya kidini, kikabila na kifamilia.