Vikwazo dhidi ya Syria vyavuruga matibabu ya Saratani
Madaktari kwenye wodi ya watoto wanaougua saratani katika hospitali ya watoto ya Damascus wanahaha kwa upungufu mkubwa wa dawa zatiba, lakini hii si tu kwa sababu ya machafuko yaliyotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe
Vikwazo vinazuia bidhaa zinazoingizwa
Miaka sita ya mzozo imesababisha huduma za afya Syria ambazo awali zilikuwa bora zaidi katika Ukanda wa Mashariki ya Kati kuwa duni kabisa. Chini ya nusu ya hospitali za nchi hiyo zinafanya kazi kikamilifu. Kiasi ya watoto 200 wanahudumiwa kwenye hospitali ya watoto ya Damascus kila wiki, huku zaidi ya asilimia 70 wakiwa wanatoka nje ya mji mkuu.
Mashirika ya nje yabakia na wasiwasi.
Watoto hawa wanaougua saratani wanasubiri matibabu katika Hospitali ya watoto ya Damascus. Maafisa wa ndani na kutoka shirika la kimataifa la afya, WHO wanalaumu vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi kwa kuzuia kabisa uingizwaji wa bidhaa za dawa, ingawa usambazaji wa vifaa tiba unaondolewa kwenye vizuizi hivyo vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya.
Kupunguzwa kwa Matumizi
Serikali ya Syria kupunguza matumizi kwenye afya na kupigana vita vinavyoigharimu kwa kiasi kikubwa, anguko kubwa la thamani ya sarafu na athari ambazo si za moja kwa moja za vikwazo kwa pamoja huzidisha mateso kwa wagonjwa wanaohitaji dawa zinazotengenezwa nje. Kabla ya vita, Syria ilizalisha asilimia 90 ya dawa zake, lakini za kuzuia saratani zilikuwa miongoni mwa zile zilizoingizwa toka nje.
Kupunguzwa bajeti ya afya ya Syria.
Wauguzi hawa huwashughulikia watoto wagonjwa. Shirika la afya duniani, WHO nchini Syria linasema, bidhaa zinazoingizwa zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na kupunguzwa kwa bajeti katika sekta ya afya tangu kuanza kwa vita mwaka 2011. Pamoja na hilo, ni anguko la asilimia 90 la Pauni ya Syria, hatua iliyochangia baadhi ya dawa kuwa na gharama za juu.
Upungufu mkubwa wa mafungu ya fedha
"Matokea ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Syria yameathiri kwa kiasi kikubwa manunuzi ya dawa maalumu ambazo ni pamoja na dawa za kuzuia saratani", amesema mwakilishi wa WHO nchini Syria, Elizabeth Hoff. "Vikwazo vilikuwa vikizuia makampuni makubwa ya kimataifa kujihusisha na serikali ya Syria pamoja na kuzuia benki za kigeni kushughulikia malipo ya dawa zinazoingizwa toka nje.
Wagonjwa wanasubiri tiba
Mgonjwa wa saratani Fahd anacheza na simu yake wakati mama yake akiwa amekaa pembeni ya kitanda. Kwa pamoja vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya vinaweka pembeni dawa na mahitaji mengine ya kibinaadamu. Hata hivyo, kutokana na kuzuiwa kwa shughuli za kifedha na biashara nyingi na serikali ya Syria, shughuli hizo kwa njia ambayo si ya moja kwa moja zinaathiri biashara ya dawa.
Kucheleweshwa kwa matibabu
Taasisi binafsi ya msaada ya Basma, inajaribu kusaidia kutoa fedha za dawa kwa ajili ya wagonjwa wa familia masikini. Kulingana na Mkurugenzi Mkuu, Rima Salem, uwiano wa wagonjwa wanaohitaji msaada umepanda kutoka asilimia 30 na kukaribia 80 tangu kuanza kwa vita. Salem anaelezea wasiwasi kuhusu kucheleweshwa tiba. "Mtoto mwenye saratani anaweza kufa akisubiri zamu yake ya kutibiwa" alisema.