1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Saudi Arabia vyashutmiwa kwa ukiukaji Yemen

25 Machi 2020

Shirika la Human Rights Watch limesema majeshi ya Saudi Arabia yamefanya ukatili mkubwa dhidi ya raia Yemen katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ikiwemo utesaji, kuwalazimisha watu kukimbia na kuwaweka kizuizini.

https://p.dw.com/p/3a1tC
Saudische Grenzkontrolle
Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Katika ripoti hiyo iliyotolewa leo shirika hilo lenye makao yake mjini New York, Marekani limeelezea hayo kutokana na ushahidi uliotolewa na wafungwa wa zamani nchini Yemen walioshikiliwa katika jimbo la al-Mahrah, ambalo linapakana na Oman na Saudi Arabia.

Raia kadhaa wa Yemen wameliambia shirika la Human Rights Watch kwamba walikamatwa na kuteswa katika kituo cha siri ambako watu wanawekwa kizuizini kwenye mji mkuu wa jimbo hilo.

Ripoti hiyo imeangazia visa 16 vya watu waliowekwa kizuizini na visa vipatavyo vitano vya wafungwa ambao walilazimishwa kuondoka kwa miezi kadhaa, na kuhamishiwa kwenye nchi jirani ya Saudi Arabia kinyume cha sheria.

Michael Page, Naibu Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika Mashariki ya Kati, anasema utesaji mkubwa uliofanywa na vikosi vya Saudia na washirika wao wa Yemen kwa wakaazi wa al-Mahra, ni janga jingine la kuongeza katika orodha ya vitendo visivyo halali vilivyofanywa na muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Hiyo ni ripoti ya hivi karibuni kuhusu ukiukaji wa haki za raia nchini Yemen ambapo zaidi ya watu 100,000 wameuawa katika vita vilivyodumu kwa muda wa miaka mitano na kusababisha nchi hiyo masikini katika ulimwengu wa Kiarabu kutumbukia katika janga la njaa.

Luftangriffe im Jemen
Vita vya Yemen vimeacha sehemu kubwa ya taifa hilo ikiwa vifusi.Picha: picture-alliance/dpa/AP/H. Mohammed

Serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa, ambayo inaungwa mkono na Saudi Arabia, iliondolewa madarakani mwaka 2014 na waasi wa Houthi wa madhehebu ya Kishia baada ya kuuteka mji mkuu, Sanaa na eneo kubwa la kaskazini mwa nchi hiyo.

Pande zote zashutumiwakwa uhalifu wa kivita

Muungano wa jeshi la Kiarabu linaloungwa mkono na Marekani lilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa ajili ya kuirejesha serikali. Mashirika ya haki za binaadamu yamezishutumu pande zote kwa kukiuka haki za kiutawala na kimfumo pamoja na uhalifu wa kivita.

Shirika la Human Rights Watch halijapokea jibu lolote kutoka kwa majeshi ya muungano yanayoongozwa na Saudia kuhusu shutuma za utesaji. Ingawa al-Mahrah iko mbali na yanakofanyika mashambulizi ya kivita nchini humo, jimbo hilo hivi karibuni limekuwa eneo la mapigano kati ya wakaazi wa eneo hilo na majeshi ya Saudi Arabia.

Saudia na vikosi inavyoviunga mkono wamewakamata raia kadhaa wa Yemen ambao wamejaa mitaani katika jimbo la al-Mahrah kupinga kuongezeka kwa uwepo wa jeshi la Saudia kwenye eneo hilo. Maandamano hayo mara kwa mara yaligeuka kuwa ya ghasia wakati ambapo majeshi yanawatawanya watu kwa kutumia risasi za moto.

Jemen Luftangriff auf Sanaa
Watoto wakikusanya vyuma kutoka kiwanda kilichohribiwa na mabomu, Januari 20, 2020.Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Wafungwa wa zamani wa Yemen wameliambia shirika la Human Rights Watch kwamba majeshi ya Yemen yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, yamewaondoa mitaani na kuwapeleka kwenye vizuizi visivyo rasmi. Wanasema wakiwa huko walipigwa na kuteswa kwa nyaya za umeme hadi pale walipokiri mashtaka ya uwongo ya kubambikiziwa na kuahidi kuachana na shughuli zote za upinzani.

Wengi wameyaelezea mazingira mabaya kwenye vituo hivyo. Mwandishi habari mmoja aliyejitambulisha kama Bassem katika ripoti hiyo, amesema maafisa wa Saudi Arabia walimtesa kwa kutumia nyaya za umeme na kumnyima chakula akiwa kwenye kituo kichafu ambacho kilikuwa kama jalala.

Akina mama wa wanaume ambao wametekwa na kuhamishiwa Saudi Arabia, wamesema miezi imepita bila ya kusikia neno lolote kutoka kwa watoto wao, lakini ghafla wanapokea simu kutoka gerezani nchini Saudia, ambako raia kadhaa wa Yemen wanaendelea kushikiliwa bila kufunguliwa mashtaka.

Page amezitolea wito serikali za Saudi Arabia na Yemen kuwaachia huru raia ambao wanashikiliwa kimakosa na zichunguze madai ya unyanyasaji ulioenea kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa.

Chanzo: Mashirika