Vijana DRC waandamana dhidi ya MONUSCO
8 Aprili 2021Siku ya Jumatano katika mji mdogo wa Kasindi, jeshi la serikali lililazimika kufyatua risasi angani, ili kuwatawanya vijana waliozuia magari ya Monusco kuingia Congo.
Katika purukushani hizo za Jumatano, watu wawili walijeruhiwa kwa risasi na mmoja kati yao alikufa kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata. Jackson Muhiwa, ambaye ni mwenyekiti wa baraza la vijana katika mji mdogo wa Kasindi amelaani tabia ya jeshi la serikali, la kuwafyatulia risasi waandamanaji.
Soma pia: Mwakilishi Maalum wa katibu Mkuu wa UN afanya ziara DRC
"Tunasikitika kuona kwamba jeshi la Congo halifanyi kazi kwa matakwa ya wananchi, kuwafyatulia watu risasi ni ishara kwamba hawajui wanachokiomba raia. Hatutaki tena uwepo wa Monusco," amesema Jackson.
Pamoja na kuwaomba vijana kuachana na maandamano na mgomo, gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Nzanzu Kasivita, aliwaomba pia vijana hao kutoyashambulia magari ya Umoja wa mataifa yanayosheheni vifaa vya kivita, ili kukabiliana na waasi.
Soma pia: UN yapendekeza mpango wa kuondoa vikosi vyake DRC
Kwa upande wake msemaji wa tume ya Umoja wa Mataifa MONUSCO nchini Congo Mathias Gilman, akiwa ametambua kwamba Monusco wako Congo kufuatia mualiko wa viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ametangaza kwamba, Monusco itaondoka nchini DRC, ikiwa serikali ya Congo itaiomba tume hiyo kuondoka.
Mathias Gilman amewakumbusha waandamanaji kwamba kuna maelfu ya wacongomani wanaopata hifadhi pembezoni mwa makambi ya Monusco na kwamba sio jambo la busara kuiomba tume hiyo kuondoka.
Soma pia: Congo yapiga hatua katika njia nzuri, asema kiongozi wa MONUSCO
"Msisahau kwamba kuna maelfu ya wacongomani wanaokimbilia pembezoni mwa makambi yetu ili kujihifadhi. Kuomba Monusco iondoke nikwenda kinyume na lengo ambalo nikustawisha amani katika eneo hili," amesema Mathias.
mapema siku ya Alhamisi, milio ya risasi bado imeendelea kusikika katika kata mbalimbali za mji wa Beni, majeshi ya serikali pamoja na polisi, wakiwa wanawatawanya waandamanaji, walio na nia ya kuvishambulia vituo vya Monusco katika kata ya Boikene.
Purukushani zinazoendelea mjini Beni, zimesababisha shughuli mbalimbali kusimamishwa, na baadhi ya shule zimefunga milango yao kwa wanafunzi isijulikane kipi kitakachotokea baadaye.