1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUturuki

Uturuki yawakamata washukiwa 189 wa kundi la kigaidi la IS

30 Desemba 2023

Polisi nchini Uturuki wamewakamata watu 189 wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye msimamo mkali wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS, katika operesheni iliyofanyika katika mikoa na miji 37.

https://p.dw.com/p/4ajJE
Türkei Ali Yerlikaya Innenminister
Waziri wa Mambo ya Ndani wa uturuki Ali Yerlikaya akiwasili kwenye sherehe za kukabidhiwa rasmi wadhifa huo mjini Ankara: 04.06.2023Picha: Arda Kucukkaya/AA/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya amesema polisi wamefanya msako kwenye nyumba zilizopo katika mji mkuu, Ankara na katika mji mkubwa wa kibiashara wa Istanbul miongoni mwa maeneo mengine, huku akichapisha picha za washukiwa hao kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.

Hayo yanajiri siku moja baada ya serikali mjini Ankara kutangaza kuwa ilizima mipango ya mashambulizi ya kundi hilo la IS dhidi ya masinagogi na Makanisa nchini Uturuki, ambayo siku za hivi karibuni yameshuhudia mashambulizi kadhaa ya kigaidi yanayohusishwa na kundi hilo la itikadi kali.

Mwaka 2017 wakati wa mkesha wa mwaka mpya, kundi la IS lilidai kuhusika na shambulio lililosababisha vifo vya watu 39 kwenye mgahawa mmoja mjini Istanbul.