1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yajitoa mazungumzo kuhusu Libya

Admin.WagnerD13 Novemba 2018

Uturuki imejitoa katika mazungumzo yanayosimamiwa na Italia kuhusu mzozo wa Libya. Uamuzi huo wa Uturuki ni pigo jengine katika juhudi za kimataifa za kurejesha utulivu katika nchi hiyo iliyogawika na kuzongwa na vurugu.

https://p.dw.com/p/38BOg
Italien Libyen-Konferenz in Palermo Fuat Oktay
Picha: picture-alliance/AA/M. Kamaci

Uturuki imetoka mazungumzoni baada ya kiongozi wa eneo la mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar kujiunga katika majadiliano  akifuatana na hasimu yake anaeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, waziri mkuu Fayez Al-Sarraj na viongozi wengine, bila ya kujumuishwa wale wa Uturuki.

Kambi ya Haftar daima imekuwa ikiituhumu Uturuki na Qatar kuwaunga mkono kijeshi na kifedha mahasimu wao ikiwa ni pamoja na makundi ya itikadi kali.

"Mkutano wowote utakaoitenga Uturuki utadhihirisha hautaleta tija katika juhudi za kusaka ufumbuzi wa tatizo lililoko" amesema Makamo wa rais wa Uturuki Fuat Oktay katika taarifa yake.

"Mazungumzo ambayo si rasmi yaliyohudhuriwa na wadau kadhaa na kuwatambulisha kama mahasimu mashuhuri yanapotoa na hayatoi picha nzuri, hali ambao tunaipinga moja kwa moja" ameongeza kusema Oktay.

Haftar awasili mkutanoni bila kutarajiwa

Khalifa Hafta Libyen
Picha: Imago/J. Mattia

Haftar amewasili mjini Palermo, mji mkuu wa jimbo la Cicilia akitokea Benghazi jumatatu usiku baada ya siku kadhaa za kutosema wazi kama angekwenda au la.Hata hivyo hakushiriki katika mkutano unaoendelea wala hafla ya chakula cha usiku jana jumatatu.

Rais Abdel Fattah al Sissi wa Misri, waziri mkuu wa Urusi, Dmitri Medvedev, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ghassan Salame, mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald Tusk na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian nao pia wameshiriki katika mazungumzo kati ya Sarraj na Haftar, chini ya usimamizi wa waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte kabla ya majadiliano yenyewe hasa ambayo yalipangwa kuijumuisha pia Uturuki.

"Inasikitisha jumuiya ya kimataifa haikufanikiwa kuleta umoja leo asubuhi" taarifa ya Uturuki imesema.

Mivutano inatatiza mazungumzo

Wadadisi wanasema mkutano wa kilele wa Palermo unakabiliwa na hatari ya kushindwa sio tu kutokana na mivutano kati ya makundi yanayohasimiana bali pia kutokana na ushawishi wa madola ya kigeni.

Libya - The Battle for Sirte - Coping with an emergency
Picha: DW/K. Zurutuza

Italia ni nchi ya karibuni zaidi iliyopania kuwaleta pamoja viongozi wa makundi yanayohasimiana baada ya mkutano wa kilele wa Paris mwezi Mei uliopita kupelekea serikali ya maridhiano ya kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli na Haftar kukubaliana uchaguzi uitishwe Disemba 10 inayokuja-tarehe ambayo sasa imeshawekwa kando.

Umoja wa Mataifa ukitambua vurugu zilizoko nchini humo tangu Muammar Gaddafi alipong'olewa madarakani na baadae kuuliwa mwaka 2011 umetangaza wiki iliyopita uchaguzi hautaweza kuitishwa kabla ya msimu wa kiangazi mwakani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga