Uturuki haitotangaza vita na Syria
4 Oktoba 2012Akizungumzia pendekezo la Uturuki kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka Syria ichukuliwe hatua za kijeshi, baada ya kombora lililorushwa kutoka mpaka wa Syria na kuwauwa raia watano katika ardhi ya Uturuki, amesema pendekezo hilo lionekane kama onyo kwa Syria.
Bunge la Uturuki hii leo linajadili kwa kina namna ya kuidhinisha uanzishaji wa operesheni za kijeshi katika maeneo ya mpaka wake na Syiria na wakati pia ikianzisha upya makabiliano kwa kutumia vifaru katika kuyakabili mashambulizi kutoka upande wa Syria.
Urusi yasikitishwa na mvutano
Katika hatua nyingine Urusi imeoneshwa kusikitishwa kwake katika kile ilichokiita hali isiyovumilika kati ya Syria na Uturuki na hasa wakati huu wa mvutano kutokana mashambulizi hayo ya mipakani. Na hatimaye kupelekea Uturuki kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi ambapo inadaiwa pia askari kadhaa wameuwawa katika eneo hilo.
Akizungumza wakati akiwa safarini nchini Pakistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kwa vile mvutano kati ya Uturuki na Syria unaendelea kwa upande wao wana jukumu kubwa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Lavrov ametoa uthibitisho kwamba Syria imesema tukio hilo halitatokea tena, na ametoa wito wa kuanzishwa kwa mawasiliano ya moja kwa moja baina ya mataifa hayo mawili ili kuweza kumaliza mzozo huo.
Kihistoria Urusi ina ushirikiano wa karibu na Syria na imekuwa ikipinga hatua ya kuingia kijeshi nchini Syria dhidi ya utawala wa rais wa nchi hiyo, Blashar al Assad, huku ikiyatuhumu mataifa ya magharibi kwa kuchochea mgogoro huo uliodumu kwa miezi 18, kwa kuacha silaha kuingizwa kwa upande wa waasi kiholela.
Hii ni mara ya kwanza kuuwawa kwa raia wa Uturuki tangu kuanza kwa vuguvugu la kumuondoa madarakani rais Assad mnamo mwezi Machi 2011.
Watu 21 wauwawa Damascus
Ndani ya Syiria kwenyewe, mripuko uliotokea baada ya majibizano ya risasi kati ya waasi na kundi dogo la wapiganaji wanaoiunga mkono serikali umesababisha watu 21 kufariki dunia mjini Damascus. Awali shirika la uangalizi wa haki za binadamu nchini humo lenye makao yake mjini London, nchini Uingereza, lilitangaza kuwa kiasi ya watu 18 wameuwawa katika eneo la Qudsaya, magharibi mwa mji huo mkuu.
Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema mapigano katika eneo la Qudsaya bado yanaendelea mpaka sasa na kwamba watu wengi wameuwawa katika mripuko wa bomu na wengine wachache katika mapambano ya risasi huku wengi wao wakiwa ni wapiganaji wanaounga mkono serikali ya Syria.
Anasema kilichobainika ni kwamba waasi wanaotumia miripuko midogo midogo walitega bomu katika makao makuu ya kikosi hicho cha ulinzi kinachoiunga mkono serikali.
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Josephat Charo