1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utumwa duniani

Abdu Said Mtullya17 Oktoba 2013

Kwa mujibu wa ripoti ya Wakfu wa "Walk Free" watu milioni 30 bado wamo katika utumwa duniani. Ripoti hiyo iliyotolewa leo inasema hali ni mbaya zaidi nchini Mauritania

https://p.dw.com/p/1A1VO
Utumwa nchini Mauritania
Utumwa nchini MauritaniaPicha: Robert Asher

Ripoti ya Wakfu wa "Walk Free," inasema wakati India ndiyo nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watumwa duniani, kiwango cha uovu huo pia ni kikubwa nchini Mauritania ambako asilimia nne ya watu wake wanasemekana kuwa wanaishi katika utumwa.

Kwa kuichapisha ripoti hiyo wakfu wa " Walk Free" unatumai kutoa mchango katika kuzisaidia serikali katika juhudi za kuufuatilia uovu wa utumwa na hivyo kuweza kuchukua hatua za kuukabili uhalifu huo uliojificha. Hata hivyo mkurugenzi wa wakfu huo Nick Grono amesema anajua kwamba serikali nyingi hazitapendelea kuyasikia hayo.

Nchi zenye kiwango cha juu cha utumwa duniani, ni pamoja na Mauritania,Haiti,Pakistan,India na Nepal. Nchi nyingine barani Afrika zenye idadi kubwa ya watumwa ni pamoja na Benin,Gambia, Ivory Coast, na Gabon.

Mkurugenzi wa wakfu wa "Walk Free" amesema watu wengi wanashangaa kusikia kwamba utumwa bado upo duniani mpaka leo licha ya utumwa uliofanyika kupitia katika bahari ya Atlantik kupigwa marufuku mnamo karne ya 18.

Ripoti ya wakfu wa "Walk Free" inasema, kwamba watu milioni 30 dunani bado wanaendelea kuathirika na utumwa. Wakfu huo umesema katika ripoti yake kwamba utumwa unaondelea leo bado unafanana na sehemu nyingi za sura ya ule wa karne zilizopita. Tafsiri ya utumwa ya Shirika la "Walk Free" , ni pamoja na utumwa mkongwe,mazingira ya kitumwa kama vile ya kunasa katika deni,ndoa za kulazimishwa na kuwauza watoto wanaotumiwa katika mazingira ya unyonyaji.Fasili ya utumwa ya asasi hiyo pia inajumlisha biashara ya kuwauza watu na kuwatumikisha kwa nguvu.

Watu wanalazimishwa kwa nguvu kufanya mambo kinyume na hiari yao.Wanakongwa au wanalazimishwa kufanya kazi na kuingizwa katika mazingira ya kunyonywa kiuchumi. Wanalipwa ujira wa kuwaezesha kuendelea kupumua tu au katika hali nyingine hawalipwi chochote na hawana uhuru wa kuondokana na mazingira yanayowakabili.

Kuhusu Mauritania Wakfu wa "Walk Free" unasema utumwa katika nchi hiyo umejichimbia katika mizizi ya kiurithi,kwa sababu watu wanaweza kuuzwa na kununuliwa ,kukodishwa au wanaweza kutolewa kama zawadi .

Mkurugenzi wa wakfu wa Walk Free, Nick Grono amesema hali ya kurithi utumwa ni ya kushtusha sana nchini Mauritania. Ameeleza kwamba watoto wanazaliwa katika utumwa nchini humo. Ameeleza kuwa wanawake na wanaume wanageuzwa watumwa na aghalabu watoto wao wanatumikishwa katika kazi za utumishi wa majumbani au wanatumikishwa katika kazi za mashambani.

Hata hivyo katika ripoti yake wakfu wa "Walk Free" umekadiria kwamba asilimia 72 ya watu waliomo katika utumwa mamboleo wako katika nchi za Asia, na India ndiyo inayoongoza. Moldova pia imo miongoni mwa nchi 10 za mbele katika orodha ya utumwa duniani. Lakini nchi hiyo pamoja na Ivory Coast zinafanya juhudi za kupambana na udhalimu huo wakati katika nchi zinazoongoza kwa utumwa duniani juhudi ni ama za kiini macho au hakuna kabisa. Nchi hizo ni Mauritania,Haiti na Paksitan. Ripoti hiyo pia imezitaja,Urusi, China,Marekani,Ufaransa na Uingereza.

Mwandishi:Mtullya Abdu./afpe,dpa,

Mhariri:Abdul-Rahman