1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado kuna mvutano wa serikali na na jeshi la Libya

19 Februari 2019

Miaka 8 tangu kutokea uasi uliofuatiwa na mapinduzi ya kumuondoa madarakani na kumuua rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi lakini uthabiti na demokrasia katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika, vinabakia kuwa ndoto.

https://p.dw.com/p/3Dcu5
Libyen Feier Jahrestag 3 Jahre ohne Gaddafi in Tripoli
Picha: Reuters

Licha ya kwamba wananchi nchini Libya walifanikiwa kuuondoa uongozi wa kiimla wa Gadaffi mwaka 2011 kupitia vuguvugu la mageuzi katika nchi za kiarabu, taifa hilo bado halijaweza kufikia uongozi bora wa kidemokrasia kutokana na machafuko ya mara kwa mara nchini humo.

Lakini raia wengi wanasema hawajutii lolote kwa kumuondoa madarakani Gaddafi aliyeongoza taifa hilo kwa muda wa miaka arobaini na nne na zaidi yake wanayo matumaini ya nchi hiyo kuwa na amani na kupata uongozi bora.

Fayez EL Sarraj
Fayez El Sarraj mkuu wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na UN Picha: Imago/Xinhua

Muhandisi katika kiwanda cha mafuta, Marwan Jalal mwenye umri wa miaka 43 anasema yanayotokea hivi sasa nchini Libya ni matokeo ya uongozi  mbaya wa Gaddafi uliodumu kwa zaidi ya miongo minne, na kuelezea matumaini kuwa kabla ya muda mrefu nchi yao itakuwa imara, japo safari hiyo itachukua muda.

"Mabadiliko yalihitajika na ilikuwa ndio nia ya kila mtu, walioongozwa na waliokuwa wakiongoza. Kila aliyeko katika uongozi, wabunge, wote walitaka mabadiliko. Kama raia tunataka mabadiliko, tulitaka kuandamana, kubeba mabango, kushangilia na kuinua bendera ya uhuru. ila madhalimu walikuwa tayari wanapanga mipango yao," alisema mmoja wa raia  Ali Mohammed al-Suaihi.

Libya imegeuka uwanja wa vita

Libya kwa sasa imesalia kuwa uwanja wa vita baina ya maelfu ya waasi na makundi ya wanasiasa wanaoongoza bila kujali sheria huku mgawanyiko ukizidi baina ya utawala na jeshi na jitihada za kuwaleta pamoja kwa ajili ya kumaliza mzozo huo zinafeli.

Mchanganuzi katika kundi la kimataifa juu ya mizozo Claudia Gazzini anasema mkakati wowote wa kumaliza mzozo wa Libya unahitaji kuhusisha siasa, usalama na uchumi na kila upande uwe na lengo moja ila hakuna njia ya moja kwa moja ya kumaliza migogoro ya kila aina iliyopo nchini humo.

Libyen Bengasi Straßenkämpfe 29.10.2014
Picha: picture-alliance/AP/Mohammed El-Sheikhy

Katika hatua za kidharura za hivi karibuni, kamanda mwenye nguvu wa vikosi vinavyodhibiti eneo la Mashariki mwa Libya Generali Khalifa Haftar alianzisha mashambulizi ya kijeshi Kusini mwa Libya ya kuwafurusha magaidi na wapiganaji wa kigeni japo hatua hiyo imezua hofu mpya na pia wachanganuzi wanaonya kwamba mashambulizi hayo yanaweza kuhatarisha kufanyika kwa mkutano wa kitaifa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kwa malengo ya kupanga uchaguzi ambao tayari umechelewa.

Ukosefu wa ustawi wa taifa hilo umewapa nafasi walanguzi wa binadamu kwa kujificha kupitia watu wengi wanaolihama taifa hilo kwenda mataifa jirani.

Zaidi, taifa la Libya kwa sasa ni taifa ambalo halina utawala wa sheria kutokana na mvutano wa uongozi baina ya serikali ya mjini Tripoli  inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na uongozi sambamba wa kikosi cha jeshi la Libya (LNA) linaloongozwa na Generali Khalifa Haftar upande wa Mashariki.

Makundi yaliyo na silaha, wapiganaji wa Jihadi na waasi wa Chad wamefanya makao katika mipaka ya Libya inayopakana na Algeria, Niger, Chad na Sudan.

Gazzini alisema pia kuna vita baina ya kabila dogo la Tubu na makabila ya kiarabu wanaopigania kuthibiti maeneo ya mipakani kwa ajili ya biashara za magendo.

Mwandishi: Faiz Musa/AFPE

Mhariri: Daniel Gakuba