1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uteuzi wa Panitchpakdi wakosolewa na nchi zilizoendelea.

Lillian Urio16 Machi 2005

Nchi zilizoendelea kiviwanda zasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amechukua uamuzi wa haraka mno kwa kumteuwa raia wa Thailand, Supachai Panitchpakdi, kuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD, lenye makao makuu mjini Geneva.

https://p.dw.com/p/CHhD
BW Supachai Panitchpakdi
BW Supachai PanitchpakdiPicha: AP

Supachai, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani sasa hivi, atashika madaraka ya kuongoza UNCTAD, mwezi wa Septemba mwaka huu. Mwanadiplomasia kutoka eneo la Kusini-Mashariki mwa Asia ameliambia shirika la utangazaji la IPS kwamba Annan ameharakisha mno uteuzi wake, miezi sita kabla, na jambo hili sio la kawaida.

Ameelezea kuwa malalamiko hayapingi uwezo wa kazi wa aliyeteuliwa bali wanalalamika kwamba hapakuwepo na kushauriana na majadiliano juu ya uteuzi. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyu, wamenyimwa nafasi hii ambao ni utaratibu wa kila mara.

Atakayeteuliwa na Annan ni lazima akubaliwe na wanachama 191 wa Baraza Kuu kabla hajapokea madaraka.

Kundi la G77, kundi kubwa ndani ya Umoja wa Mataifa limeliomba Baraza Kuu kusubiri siku 30 kabla ya kumpigia kura mteuzi wa Annan. Matokeo yake mpango wa kupiga kura uliotakiwa kufanyika wiki ilyopita umesogezwa, hadi mwezi ujao.

Kwa kawaida mteuliwa wa Annan, kwa kazi za ngazi za juu za Umoja wa Mataifa, huwa anakubaliwa na Baraza Kuu, hadi leo hamna aliyekataliwa. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 60 kwa Baraza Kuu kuomba muda ili kumpigia kura mteuliwa wa Katibu Mkuu.

Balozi Stafford Neil wa Jamaica, mwenyekiti wa G77, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wameomba muda zaidi ilikujadiliana kwa sababu UNCTAD ni muhimu sana kwa G77.

Kundi la G77, lililoundwa mara baada ya kuanzishwa kwa UNCTAD mwaka 1964, limekuwa likifanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa kwa miaka 40. Nchini Brazil mwezi wa Juni mwaka jana, Jumuiya zote mbili zilisherekea miaka 40 tangu kuundwa.

Ingawa Supachai ni raia wa Thailand, serikali ya Thailand imejitenga na uteuzi wake. Balozi Laxanachantorn Laohaphan wa Thailand ameliambia shirika la habarai la IPS kwamba Supachai sio mteuzi wa serikali ya Thailand. Alitaka kufafanua kwamba kuna wagombea wengine kutoka Asia wanaotaka nafasi hii na utawala wa Thailand haudhamini uteuzi wa Supachai.

Wagombea wengine wa kazi hiyo ya UNCTAD ni pamoja na raia kutoka Cambodia, Philippine, Pakistan na Bangladesh. Annan aliwahi kutangaza uteuzi wake na kutangulia nchi nyingine kujaribu kushawishi wagombea wao kupata nafasi ya kuteuliwa.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia, serikali ya Thailand haijafurahishwa na uteuzi huu kwa sababu unaweza kuikosehsa nafasi ya raia mwningine wa nchi hiyo kupata wadhifa wa juu zaidi katika Umoja huo, wadhifa wa Katibu Mkuu.

Mgombea rasmi kutoka Thailand wa nafasi hiyo ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Surakiat Sathirathai, ambaye sasa hivi ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu msaidizi katika upangaji mpya wa mawaziri uliofanyika Bangkok wiki iliyopita.

Uteuzi wa Surakiat umedhaminiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki, Malaysia, Philippines, Singapore, Thailand, Indonesia, Brunei, Burma, Vietnam, Cambodia na Laos.

Kama Supachai atakubaliwa na Baraza Kuu, basi itakuwa vigumu kwa raia mwingine kutoka Thailand kugombania nafasi ya juu ya Umoja huo. Kwa kipindi cha miaka 34 hajakuwepo Katibu mkuu kutoka bara la Asia, baada ya Thant, kutoka Burma. Sasa nchi za Asia zinawania nafasi itakayotokea baada ya Annan kumaliza awamu ya pili ya miaka mitano Desemba mwaka 2006.