1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi hamkani Mali

28 Machi 2012

Viongozi wa kijeshi nchini Mali wamesema wameidhinisha katiba mpya-saa 48 kabla ya ziara ya viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika Magharibi wanaoshikilia katiba iheshimiwe haraka nchini humo.

https://p.dw.com/p/14TFZ
Wanajeshi walionyakua madaraka MaliPicha: Reuters

Baraza la taifa kwaajili ya kuimarisha demokrasia ,limepitisha "sheria msingi"-katiba ya vifungu 70 itakayotumika katika kipindi cha mpito"-hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na mwanajeshi mmoja kupitia televisheni ya serikali.

Dibaji ya sheria hiyo msingi inazungumzia juu ya dhamiri ya umma wa Mali kuwa na taifa linaloheshimu sheria na demokrasia ya vyama vingi na ambako haki za kimsingi za binaadam zinaheshimiwa.

Hakuna hata mwanachama mmoja wa baraza la kijeshi na serikali yake itakayoundwa baadae,atakaeruhusiwa kupigania kiti bungeni au wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa-taarifa hiyo imesemna bila ya kutaja lakini lini uchaguzi huo utaitishwa ,wala kwa muda gani kipindi cha mpito kitadumu.

Ecowas Treffen in Abuja Ouattara
Rais wa Côte d'Ivoire Alassane Ouattara (kati)Picha: Reuters

Katika kipindi chote cha mpito,baraza la kijeshi ndilo litakalokuwa na usemi na kiongozi wake Amadou Sanogo,ndie kiongozi wa taifa atakaeunda serikali.

Wanajesghi wamempinduwa rais Amadou Toumani Toure,(ATT),wiki chache tu kabla ya uchaguzi wa rais uliokuwa uitishwe April 29 mwaka huu.

Tangazo la katiba mpya limetolewa katika wakati ambapo mkutano wa dharura wa viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi umeamua mjini Abidjan kutuma ujumbe wa viongozi wa taifa kudai katiba iheshimiwe haraka nchini Mali.

Ujumbe huo wa marais sita, utaongozwa na rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire,mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi ECOWAS.Miongoni mwa marais hao ni pamoja na rais wa Liberia,bibi Ellen Johnnson Sirleaf,Goodluck Jonathan wa Nigeria na Blaise Compaore wa Bourkina Fasso aliyechaguliwa kuwa mpatanishi wa mzozo wa Mali.

Amepewa jukumu la kuanzisha mazungumzo ya maana pamoja na pande zote ili kurejesha amani nchini.Pindi juhudi hizo zikishindwa,jumuia ya ECOWAS itachukua hatua zinazostahiki kumaliza uasi-viongozi wa ECOWAS wamesema.

Jumuia ya ECOWAS imeruhusu pia vikosi vyake vya kijeshi viwekwe tayari ili kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza,wamesema viongozi waliohudhuria mkutano wa Abidjan waliotaka silaha ziwekwe chini kote nchini Mali ambako waasi wanaendelea na mapigano katika eneo la kaskazini.

Alltag in Malis Hauptstadt Bamako
Harakati za maisha katika mji mkuu BamakoPicha: DW

Baada ya kuamuru ofisi na maduka yafunguliwe ,viongozi wa utawala wa kijeshi wametangaza pia kubatilishwa sheria ya kutotoka usiku na kufunguliwa mipaka ya nje ya nchi hiyo.

Wagombea wawili wa kiti cha rais,waziri mkuu wa zamani Modibo Sidibé na mfanyabiashara Jamil Bittar wameachiwa huru na wanajeshi wanaowashikilia pia watu wengine 12 mashuhuri.

Vuguvugu dhidi ya mapinduzi,linalovileta pamoja vyama kadhaa pamoja na mashirika ya huduma za jamii limeelezea azma ya kutaka kuzungumza haraka pamoja na wanamapindizui ili kurejesha hali ya kawaida nchini.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman