1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakataa pendekezo la kubadilishana maeneo na Ukraine

12 Februari 2025

Urusi hii leo imepinga mpango wa kubadilishana maeneo yanayokaliwa na Ukraine, kama sehemu ya mpango wowote ujao wa amani, masaa machache baada ya kuivurumishia Kyiv mkururo wa makombora na droni na kumuua mtu mmoja.

https://p.dw.com/p/4qNUA
Urusi |  Dmitri Peskow
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba Urusi haijawahi na kamwe haitafanya majadiliano kuhusiana na kubadilishana maeneo na Ukraine.

"Dmitry Peskov: Hili haliwezekani. Urusi hijawahi kujadiliana na kamwe haitajadiliana na Ukraine suala hili la kubadilishana maeneo. Na, kwa hakika vikosi vya Ukraine vitafukuzwa kwenye maeneo hayo. Kila mmoja ambaye hataangamizwa, atafukuzwa."

Soma pia:Zelensky: Ukraine iko tayari kubadilishana eneo la ardhi na Urusi
                    
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliyetoa hoja hiyo amesema mashambulizi haya ya karibuni yanaonyesha Urusi haiko tayari kwa mazungumzo ya amani na Ukraine. 

Ameandika kwenye mtandao wa X kwamba Rais Vladimir Putin hayuko tayari kwa amani, kwa kuwa anaendelea kuwaua Waukraine na kuharibu miji.