1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaendeleza mashambulizi yake kwenye mji wa Odessa

20 Julai 2023

Urusi imefanya mashambulizi mengine ya anga usiku wa kuamkia leo (20.07.2023) kwenye mji wa mwambao wa Bahari Nyeusi wa Odessa nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4U9S2
Ukraine ikishuhudia uharibifu uliofanywa na hujuma za Urusi kwenye mji wa Odessa
Mashambulizi ya Urusi kwenye maeneo kadhaa ya mkoa wa Odessa yamesababisha moto.Picha: Cover-Images/IMAGO

Mashambulizi hayo ya kutumia makombora ya masafa na ndege zisizo na rubani yameutikisa mji huo wa kusini mwa Ukraine kwa siku ya tatu mfululizo. Hujuma hizo zinatajwa kuwa ndiyo kubwa zaidi kufanywa na Moscow dhidi ya mji huo ulio lango la usafirishaji nafaka za Ukraine chini ya mkataba na Urusi ambao yumkini umesambaratika.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti milio mizito ya makombora usiku kucha huku mifumo ya ulinzi ya anga ya Ukraine ikijaribu kupambana kuyaangusha.

Jeshi la Ukraine limesema vituo vya kijeshi na miundombinu mingine imelengwa na kwamba kwa jumla Urusi ilivurumisha kiasi makombora 31 ya aina tofauti na mengi kati ya hayo hayakuweza kudunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Hata hivyo kati ya ndege ziszo na rubani 32 zilizorushwa na vikosi vya Moscow, 23 ziliangushwa na jeshi la Ukraine.

Hujuma pia zimeilenga miundombinu ya bandari za mji huo ambazo ndiyo zimekuwa lango la usafirishaji mazao ya nafaka kutoka Ukraine chini ya mkataba ambao sasa umeingia kiwingu baada ya Urusi kutangaza kujitoa mapema wiki hii.

Rais Zelensky asema maelfu ya tani za chakula imehariwa 

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine Picha: Georgi Paleykov/NurPhoto/picture alliance

Ukraine imesema kituo cha kupokea na kupakia nafaka kimeshambuliwa na ghala la kuhifadhi mafuta ya kupikia yanayosafirishwa nje ya Ukraine pia limehujumiwa. Katikati mwa mji wa Odessa, majengo ya kuhifadhi mazao yamelengwa na kuharibiwa na mashambulizi hayo yamesababisha moto uliosambaa kwenye eneo la ukubwa wa mita za mraba 3,000.

Kupitia hotuba yake ya kila siku kwa umma, rais Volodomyr Zelensky ametoa takwimu za uharibifu uliotokea akisema kiasi tani 60,000 za nafaka zimeharibiwa kutokana na mashambulizi hayo ya Urusi.

Amearifu kuwa shehena hiyo ilikuwa imepangwa kusafirishwa kwenda nje na ametahadharisha matendo hayo ya Urusi haiyaigharimu Ukraine pekee bali ulimwengu mzima

"Shambulizi hili (huko Odessa) linathibitisha kuwa shahaba siyo Ukraine pekee na siyo dhidi ya maisha ya watu wetu. Karibu tani milioni moja ya chakula iliyokuwa imehifadhiwa ilishambuliwa hii leo. Hiyo ni shehena ambayo ilipaswa kupelekwa kwa walahi wa mataifa ya Afrika na Asia muda mrefu uliopita", amesema Zelensky.

Mbali ya mji huo, Urusi pia imeshambulia mji mwingine wa Mykolaiv ikililenga eneo la katikati ikwemo jengo moja la maakazi ya watu ambalo lilishika moto.

Gavana wa mji huko, Vitaliy Kim, amesema watu tisa wamejeruhiwa kwenye mfululizo huo wa mashambulizi. Mji wa Mykolaiv unapakana na pwani ya Bahari Nyeusi kiasi kilometa 170 kutoka rasi ya Crimea iliyonyakuliwa kwa mabavu na Urusi mwaka 2014.

Urusi yatuma onyo kwa meli zinazopita kwenye Bahari Nyeusi 

Katika hatua nyingine Urusi imesema kuanzia sasa itazingatia meli zote za mizigo zinazokwenda nchini Ukraine kupitia Bahari Nyeusi kuwa kitisho kwa usalama wake na inaweza kuzishambulia.

Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imesema vyombo hivyo vinavyoelekea kwenye bandari za Ukraine vitazingatiwa na Moscow kuwa vimebeba shehena ya silaha na mataifa yanayozimiliki yatakuwa yamejiingiza kwenye vita vya Ukraine na yapo upande wa serikali ya Kyiv.

Tamko hilo la Urusi linafuatia uamuzi wake wa siku ya Jumatatu wa kujitoa kutoka kataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine kupitia bandari za bahari nyeusi.

Ukraine kwa upande wake imezirai nchini nyingine kwenye kanda ya Bahari Nyeusi kuingilia kati na kuhakikisha usalama wa meli zote zinazotumia ujia huo wa maji.