1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi haijavutiwa na mapendekezo ya mazungumzo ya amani

10 Februari 2025

Urusi bado haijapokea mapendekezo ya kuvutia kuanza mazungumzo kuhusu Ukraine.

https://p.dw.com/p/4qG8Z
Ukraine | Sibirisches Bataillon
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Haya ni kulingana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Mikhail Galuzin katika matamashi yaliochapishwa leo baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba anaamini nchi yake ilikuwa inapiga hatua ya kumaliza vita nchini Ukraine.

Katika mahojiano, Galuzin ameliambia shirika la habari la serikali RIA kwamba ni muhimu maneno yaambatane na vitendo vinavyozingatia maslahi halali ya Urusi, kuonyesha utayari wa kutokomeza sababu za msingi za mgogoro na kutambua ukweli mpya.

Wikendi iliyopita, Trump alisema kuwa amezungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kwamba anatarajia mazungumzo zaidi kufanyika.

"Lazima tumalize vita. Vitaisha. na lazima tuvimalize. Havikupaswa kutokea, havingetokea kama ningekuwa rais," alisema Trump.

Hapo jana, msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, ameliambia shirika la habari la TASS kwamba mawasiliano mengi yanajitokeza kuhusu mazungumzo kati ya Putin na Trump na kwamba hawezi kufahamu kila kitu.