1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wadai kutotendewa kwa usawa

Admin.WagnerD26 Agosti 2020

Kumekuwa na mlolongo wa matukio ya wagombea wengi wa upinzani wa nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha.

https://p.dw.com/p/3hWai
Afrika Tansania Präsidentschaftswahlen 2020
Picha: DW/S. Khamis

Hali iliyowafanya baadhi ya wagombea wa CCM kupita kabla ya hata ya uchaguzi wenyewe kufanyika. 

Ripoti zinasema baadhi ya wagombea wa upinzani walikumbana na matukio ya kutekwa, kuvamiwa na wengine kuenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali. Karibu vyama vyote vya upinzani vimekuwa vikitoa matamko ya kulaani na kukemea hali hiyo.

Mbali na hilo vyama hivyo vimeanza michakato ya kuyakatia rufaa maamuzi yaliyotolewa na wasimamizi wa uchaguzi wanaolalamikiwa kuziendea kinyume sheria zinazozimamia uchaguzi huo.

Miongoni mwa vyama ambavyo vimetoa msimamo wa kusonga mbele yaani kukata rufaa hiyo ni pamoja na chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho baadhi ya wagombea wao wanadaiwa kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Tansania | Wahlen | Wahlstimmen werden abgegeben
Baadhi ya wagombea inadaiwa wameenguliwa na wasimamizi wa uchaguziPicha: DW/E. Boniphace

Chama hicho kimeanza kukusanya taarifa kutoka kwa wagombea wake kwa shabaha ya kuhoji uhalali iliotumika kuwapiga kalamu nyekundu wagombea wake. Hali kama hiyo pia inatajwa kuchukuliwa na vyama vingine ikiwamo Chama cha Wananchi CUF.

Mkurugenzi wa uenezi na itikadi wa chama hicho, Mohammed Ngulangwa amesema CUF imevunjwa moyo na namna wagombea wa upinzani walivyotendewa katika hatua ya mwisho ya urejeshaji wa fomu.

Tansania Wahlkampf Oppositionspartei ACT Wazalendo
Chama cha ACT Wazalendo nacho kimedokeza uwezekano wa kukata rufaa na tayari kimelaani vitendo hivyoPicha: DW/E. Boniphace

Chama kingine cha upinzani cha ACT Wazalendo ambacho nacho wagombea wake wamekumbana na hali hiyo kimedokeza uwezekano wa kukata rufaa na hii leo kilikuwa kimepanga kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia mambo hayo hayo ya uchaguzi. Mgombea wake wa Urais, Bernard Membe tayari ametoa kauli ya kulaani vitendo hivyo.

Kumekua na ripoti kuwa baadhi ya wagombea walioenguliwa kwenye mchakato huo walikosea kufuata vipengele kadhaa wakati wa ujazaji wa fomu zao za uteuzi. Hata hivyo, Mkurugenzi wa idara ya habari na elimu ya mpiga kura kwa umma, Giviness Aswile wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Taifa TBC, alisemakuwa tume hiyo ilikuwa ikusubiri kupata ripoti kutoka kwa watendaji wake walioko mikoani.

Kulingana na sheria ya uchaguzi, wagombea wote wenye nia ya kutaka kukata rufaa wanao muda wa kufanya hivyo kuanzia jana jioni hadi leo saa kumi jioni. Maamuzi yanayotolewa na tume ya uchaguzi kuhusiana na rufaa zote zilizokatwa hayawezi kuhojiwa wala kupingwa na ngazi nyingine yoyote.

Amesema tume hiyo huenda ikaanza kuzitathmini changamoto zote zilizojitokeza kutoka kwa timu yake ilyoko mikoani baada kupokea taarifa. 

Mwandishi: George Njogopa