UN: Hali inazidi kuwa mbaya Ukanda wa Gaza
18 Mei 2021Msemaji wa Ofisi ya Msaada wa Kiutu ya Umoja wa Mataifa, Jens Laerke, amesema hadi kufikia leo karibu Wapalestina 47,000 wamezihama nyumba zao baada ya zaidi ya wiki nzima ya mashambulizi makali ya anga yanayofanywa na jeshi Israel.
Kundi la Hamas linaloongoza Ukanda wa Gaza nalo limejibu kwa kufyetua zaidi ya maroketi 3,400 kuelekea Israel katika kipindi hicho tangu kuanza kwa machafuko.
Laerke amesema Ukanda wa Gaza sasa unakabiliwa na upungufu mkubwa wanishati ya umeme inayopatikana kwa saa sita hadi na nane pekee kwa siku nzima.
Akinukuu duru kutoka mamlaka za Palestina, afisa huyo amesema majengo 132 yanayojumuisha makaazi 621 pamoja na ofisi za biashara yameporomoshwa kwa mabomu kwenye Ukanda wa Gaza huku nyumba nyingine 316 zimeharibiwa kabisa na hujuma za mashambulizi ya ndege za Israel.
Msaada washindwa kupelekwa Ukanda wa Gaza
Hayo yaanarifiwa wakati leo msaada uliopangwa kupelekwa Gaza umeshindwa kuwasili kutokana na mashambulizi kwenye maeneo mawili ya kuingia kwenye ukanda huo.
Israel imesema vituo viwili vinavyotumika kama njia ya kuingia Gaza vilifunguliwa kwa muda kuruhusu msaada wa vifaa vya matibabu na mafuta kupelekwa ndani ya ukanda huo lakini vilishambuliwa kwa maroketi.
Taarifa ya Israel imesema mwanajeshi wake mmoja amejeruhiwa na kufuatia mashambulizi hayo uamuzi umefikiwa wa kusitisha msafara wa malori uliokuwa unapeleka msaada huko Gaza.
Mashambulizi hayo kwenye vituo vya mpakani vya Kerem Schalom na Erez yamejiri baada ya wapiganaji wa kundi la Hamas kuanza tena kuvurumisha maroketi kuelekea Israel baada ya kusitisha kwa saa sita.
Jeshi la Israel limesema limeendeleza kampeni yake ya mashambulizi ya anga kwa kuyalenga makaazi ya viongozi wa kundi la Hamas.
Wakati hayo yakijiri maelfu ya watu wameandamana mjini Ramallah, maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi na nchini Israel kulaani hujuma zinazofanywa na jeshi la Israel huko Gaza.
Maandamano yafanyika katikati ya miito ya kusitishwa mapigano
Mjini Ramallah, maelfu ya Wapalestina walihudhuria maandamano hayo huku wengi wakibeba mabango yaliyosomeka "Kuwapiga watoto mabomu siyo hatua ya kujilinda”
Katika hatua nyingine mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya leo wamejadili jinsi ya kutumia ushawishi wa kanda hiyo kumaliza mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Kipalestina.
Umoja huo umechukua msimamo wa pamoja wa kutoa miito ya kusitishwa mapigano huku ukihimiza kutafutwa suluhu ya kudumu kwa mzozo wa huo wa Mashariki ya Kati.
Tangu kuanza kwa mapigano Wapalestina 212 na Waisraeli 12 wamekufa na maelfu ya watu wengine wamejeruhiwa wengi wakiwa ni kutoka Ukanda wa Gaza.