EU watoa wito kwa pande hasimu Libya kuweka silaha chini
9 Januari 2020Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa chini ya usimamizi wa Fayez al-Sarraj inakabaliwa na mapambano kutoka kwa vikosi vya upinzani vinavyodhibiti eneo la Mashariki mwa nchi hiyo na kutokana na hali hiyo, balozi wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amefanya mazungumzo na Fayez kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu kabla hali haijakuwa mbaya zaidi.
Fayez pia amekutana na Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas kuzungumzia mustakabali wa Libya.
Viongozi hao wamewaambia wanahabari kuwa wanataka kuizuia Libya kuwa uwanja wa mapambano na sehemu ya umwagikaji wa damu kama ilivyo Syria kwa sasa.
Heiko Maas amesema, "Waziri mkuu wa Libya Fayez Al Serraj anaunga mkono mazungumzo ya Berlin, na pia amesema ataridhia maafikiano yoyote ambayo yatakubaliwa kwenye mkutano huo".
Kauli za viongozi hao wa Umoja wa Ulaya zinajiri baada ya vikosi vya mbabe wa kivita Khalifa Haftar ambavyo vinapata uungwaji mkono wa Misri, Umoja wa Milki za kiarabu UAE na Urusi, vilivyochukua udhibiti wa mji wa Pwani wa Sirte.
Hatua ya mbabe huyo wa vita inalenga kuchukua kabisa udhibiti wa mji wa Tripoli na pia kumuondoa mamlakani Fayez.
Katika taarifa ya pamoja, Umoja wa Ulaya umeahidi kuongeza juhudi za mapatanisho ya kisiasa kati ya vikosi hasimu nchini Libya.
Maas, ambaye siku moja kabla alifanya mazungumzo ya dharura kuhusu kadhia ya Libya na Ufaransa, Uingereza na Italia, amesema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha maelewano yataafikiwa katika mkutano wa Berlin ambao umepangwa kufanyika mjini Berlin na kufadhiliwa na Umoja wa Mataifa.
Pia katika juhudi za kuongeza kasi ya mapatanisho kati ya pande hasimu, waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte alifanya mazungumzo na Haftar mjini Rome na kumtolea wito wa kuweka silaha chini. Conte ameonya kuwa vita vinavyoendelea nchini Libya huenda vikachangia ukosefu wa utulivu wa eneo pana la Libya.
Aidha hakuna tarehe iliyowekwa kwa ajili ya mkutano wa Berlin, lakini Maas amesema kuwa huenda mkutano huo ukafanyika katika wiki chache zijazo.
Wakati huo huo, Borrell ameikosoa Uturuki kwa kuingilia kati mzozo wa Libya, akisema hali hiyo huenda ikachochea zaidi mivutano. Hata hivyo, Ankara imesema nia ya kutuma wanajeshi 35 nchini Libya ni kutoa mafunzo na kuiunga mkono serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, na wala sio kushiriki vita.
Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel wikendi hii anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan huku nae Borrell akipanga kukutana na viongozi wengine wa Libya akiwemo Haftar ili kutafuta utatuzi.
Vyanzo/AFP/APE