Umoja wa Ulaya waionya Uingereza kuhusu mktaba wa Brexit
9 Septemba 2020Umoja wa Ulaya umeionya Uingereza kwamba ina wajibu wa kuheshimu makubaliano ya kujiondowa, ambayo yanapaswa kuweka misingi kuhusu uhusiano wa baadaye. Kwa upande wake Ujerumani na Ufaransa zinasubiri utekelezwaji kamili wa mkataba wa Brexit. Kauli hizo zimetolewa baada ya Uingereza kukivunja kifungu muhimu cha mkataba wa Brexit.
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema hatua yoyote ya Uingereza ya kubadili kifungu cha makubaliano ya Brexit itakiuka sheria ya kimataifa na masharti yaliyopo kuhusu uhusiano wa baadaye.
Kwenye mtandao wake wa Twitter, Von der Leyen amesisitiza kwamba msingi wa makubaliano ya Brexit unatakiwa kuheshimika na mkataba huo kuendelea kutekelezwa kama ulivyo.
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya pia imesema kwamba iko tayari kufikia haraka makubaliano na Uingereza kuhusu uhusiano wa baadaye wa kiuchumi na kibiashara lakini pia umoja huo umesisitiza kwamba makubaliano hayo yatapaswa kuhakikisha haki na ushindani huru.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliipigia debe bungeni hatua ya serikali yake ya kukiuka baadhi ya vipengele vya makubaliano ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Mageuzi hayo yaliotangazwa leo Jumatano yalielezewa na Boris Johnson kwamba yanalenga kurahisisha na usalama wa biashara vya ndani nchini Uingereza.
''Kazi yangu ni kudumisha uadilifu wa Uingereza lakini pia kuulinda mchakato wa amani wa eneo la Ireland ya Kaskazini na makubaliano ya Ijumaa Kuu. Na kwa kufanya hivyo tunahitaji kuilinda nchi yetu dhidi ya siasa kali au tafsiri za kiitikadi zitakazosababisha utengano katika eneo la mpakani.''
Boris Johnson amesema mageuzi hayo yanalenga kuyabadilisha makubaliano yaliyofikiwa kuhusiana na Ireland ya Kaskazini na msaada wa serikali.
Johnson akosolewa ndani ya serikali yake
Hata hivyo, Jonson anakosolewa hata ndani ya serikali yake mwenyewe. Brandon Lewis, waziri anayehusika na maswala ya Ireland ya Kaskazini, amesema kwamba mageuzi ya upande mmoja kwa mkataba wa kimataifa yanakiuka sheria ya kimataifa.
Spika wa bunge la Ulaya, David Sassoli amesema kwamba ukiukaji wa mkataba huo umeiweka Uingereza katika athari kubwa kutoka kwa Umoja wa Ulaya.
Naibu waziri mkuu wa wa Ireland, Leo Varadkar, alifananisha jaribio hilo la serikali ya Uingereza kama kitendo cha kujitoa muhanga ambacho madhara yake yanamrejelea mhusika.
Ujerumani yaelezea wasiwasi wake
Naibu waziri wa Ufaransa anayehusika na maswala ya Ulaya, Clement Beaune amesema kwamba wana nia nzuri kwa ajili ya mazungumzo hayo lakini watakuwa na msimamo wa dhati. Aliyasema hayo baada ya mashauriano na mwenzie wa Ujerumani Michael Roth, mjini Berlin.
Maria Adebhar, msemaji wa wizara ya mamabo ya nje ya Ujerumani amesema Ujerumani inasubiri kuona Uingereza inaendelea kutekeleza mkataba wa Brexit.