Umoja wa Mataifa watoa wito kuwahifadhi wahamiaji 200,000
5 Septemba 2015Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi leo limeutolea wito Umoja wa Ulaya, kuwakubali wahamiaji 200,000 kama sehemu ya mpango wa uhamishaji wa wimbi la wahamiaji, jukumu ambalo nchi wanachama wa umoja huwo watashurutishwa kugawana.
Kamishna Mkuu Antonio Guterres wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa yake kwamba wahamiaji wenye madai ya kweli ya kutafuta hifadhi ya ukimbizi, lazima wanufaike na mpango huu maalumu wa uhamisho wa wahamiaji, na kwa ushirikiano wa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Aliongeza kuwa makisio ya awali yanaonesha kuwa takriban wahamiaji 200,000 wanahitaji sehemu za hifadhi.
Wito wa Guterres umekuja kabla ya mkutano wa mawaziri wa nchi za nje wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika baadae leo kujadili mgogoro wa wahamiaji uliolikumba bara hilo, ambao umezidi kuzusha mijadiliano duniani kote baada ya picha ya maiti ya mtoto mdogo wa kiume Aylan Kurdi inayomuonesha kutupika kifudifudi katika ufukwe wa Uturuki kusambaa katika mitandao ya kijamii wiki hii.
Nchi za Ulaya kugawana wahamiaji
Akiizungumzia picha hiyo Guterres amesema bara la Ulaya haliwezi tena kushughulikia mgogoro wa wahamiaji kwa hatua za pole pole. Aliongeza kuwa hamna nchi inayoweza kubeba mzigo huu pekee na hamna nchi inayoweza kukimbia kubeba sehemu ya mzigo huu.
Wito wake unalingana na ule wa Ufaransa na Ujerumani wa kuutaka Umoja wa Ulaya kuweka sheria itakayolazimisha kugawanywa kwa wahamaiaji hao kwa kila nchi ya Umoja huo. Mgogoro wa wahamiaji zaidi umeziathiri Ugiriki, Italia na nchi nyengine za kusini-mashariki pamoja na Ulaya ya kati, ambazo wahamiaji huwo wanapitia kuelekea Ulaya ya magharibi.
Duru za Ulaya zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker atazindua rasmi mpango wa usafirishaji wa takriban wahamiaji wengine 120,00 wiki ijayo.
Wakati huo huo nchini Hungary mamia ya wahamiaji ambao kwa siku kadhaa sasa wamekwama katika kituo cha treni cha Keleti mjini Budapest, wameanza kukusanya mizigo yao na kusema kuwa watatembea kwa mguu hadi Vienna, mji mkuu wa Austria.
Kwa siku kadhaa sasa mamalaka nchini Hungary zimekuwa zikiwazuia wahamiaji hao kusafiri na kuelekea Austria na Ujerumani, nchi ambazo wahamiaji hao ndipo wanapotaka kuenda.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef