1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa lapitisha azimi la vikwazo kwa Sudan Kusini

4 Machi 2015

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la vikwazo dhidi ya Sudan Kusini lakini likasita kuweka vikwazo vya silaha, marufuku ya kusafiri na kuzuiwa kwa mali za maafisa wa Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/1Ekgd
Südsudan Juba Militär 02/2015
Picha: picture-alliance/AA/S. Bol

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani linaunda kamati ya vikwazo itakayowasilisha kwa baraza la usalama majina ya wale wanaohujumu usalama, kuvuruga mchakato wa kutafuta amani, kuzuia usambazaji wa misaada ya kibinaadamu, kuwasajili watoto jeshini au kuwashambulia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Watu hao watatakiwa kuadhibiwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa ikiwemo marufuku ya kusafiri na mali zao kuzuiwa.

Wapatanishi wa Shirika la Maendeleo la Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, wamempa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar hadi kesho Alhamisi kufikia makubaliano ya mwisho kumaliza vita vya miezi 14.

Kufikia sasa juhudi za shirika hilo kujaribu kumaliza vita vya wenyewe zimegonga mwamba, huku watu wapatao 10,000 wakiwa wameuwawa na wengine milioni 1.5 wakilazimika kuyakimbia makazi yao. Duru ya sasa ya mazungumzo ya IGAD inatarajiwa kukamilika kesho mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo waasi walionya jana huenda yakafeli kama serikali haitakubali suala la kugawana madaraka katika serikali ya umoja wa kitaifa itakayoundwa.

UN Sicherheitsrat IS Samantha Power 15. August
Samantha PowerPicha: DON EMMERT/AFP/Getty Images

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power alisema anatumai kuwa na azimio hilo, liloweka muda kwa mujibu wa juhudi za IGAD za kuusuluhisha mzozo wa Sudan Kusini, kutaimarisha fursa za IGAD kufanikiwa kupata amani ya kusadikika na ya kudumu.

"Tunaimarisha uwezo wa IGAD katika mazungumzo kwa kutuma ujumbe wa wazi kwa wale wanaoendelea kuchagua vita badala ya amani. Mtabebeshwa dhamana sasa, tunapowahimiza mkubaliane na baadaye mtakapokuwa mkitafakari kama mtafuatilia kanuni za makubaliano hayo."

Azimio lakosolewa

Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa Francis Deng alilikosoa vikali azimio hilo. "Kama inavyosemwa mara kwa mara, lengo si kuwalenga viongozi wa ngazi ya juu, bali watu binafsi wa ngazi ya wastani ambao huenda hawana jukumu muhimu katika mchakato wa amani, adhabu ya aina hiyo huenda isilete tija."

Balozi huyo aidha alisema, "Kwa upande mwingine kuwaadhibu watu wenye majukumu muhimu katika mchakato wa amani kwa wakati huu huenda kukasababisha matokeo mabaya kwa juhudi za amani."

Bildkombo Südsudan Riek Machar und Salva Kiir
Rais Salva Kiir (kushoto) na Riek MacharPicha: Getty Images/Zacharias Abubeker/Ashraf Shazly/Montage

Azimio hilo lilipitishwa na wanachama wote 15 wa baraza la usalama, ikiwemo China, ambayo balozi wake Liu Jieyi alikuwa amehoji umuhimu wa vikwazo akisema havifai wakati huu pande zinazohasimiana zikiendelea na mazungumzo magumu.

Wanadiplomasia wamesema hatua hiyo ya kuelekea vikwazo iliungwa mkono na wanachama wote baada ya serikali za mataifa ya Afrika yaliyokatishwa tamaa na kukosekana ufanisi katika mazungumzo ya amani, kuiunga mkono.

Mjumbe wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Pyotr Ilyichev, ameelezea wasiwasi wake akisema hatua hiyo huenda imefanywa haraka na vikwazo huenda visisaidie juhudi za kutafuta amani.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Wastch, Philippe Bolopion, amelikosoa azimio hilo kwa kutojumuisha kikwazo cha silaha.

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/AFPE/APE

Mhariri:Daniel Gakuba