Umoja wa Mataifa waonya juu ya mapigano magharibi mwa Darfur
27 Aprili 2024Umoja huo umeonya kwamba shambulizi lolote linaweza kuwa na matokeo mabaya kwa wakaazi 800,000 wa jiji hilo na kuongeza kuwa vikosi vinayopigana nchini humo vya SAF na RSF hivi sasa vinajipanga upya.
Ofisi ya umoja huo ya misaada ya kiutu, imesema jana kwamba kuongezeka kwa mapigano karibu na mji El Fasher, Kaskazini mwa Darfur wiki mbili zilizopita yamewafanya watu 40,000 kukimbia, na wengi kujeruhiwa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu Antonio Guterres kwa mara nyingine alitoa wito kwa pande hizo kujizuia kupigana katika eneo la Kaskazini la Darfur karibu na mji mkuu wake, El Fasher.
Mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja huo Rosemary DiCarlo alisema Ijumaa iliyopita kwamba vita hivyo vinavyochochewa na msaada wa silaha kutoka nje na kudumu kwa mwaka mmoja sasa vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu.