1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika watangaza jopo la Ivory Coast

Abdu Said Mtullya31 Januari 2011

Umoja wa Afrika umewateua marais watano watakaolishughulikia tatizo la Ivory Coast.

https://p.dw.com/p/1082F
Viongozi wa Umoja wa nchi za Afrika.Picha: picture-alliance/ dpa

Viongozi wa nchi za Afrika leo wameyatangaza majina ya jopo la marais watakaoushughulikia mgogoro wa kisiasa wa nchini Ivory Coast. Uamuzi wa kuunda jopo hilo umefikiwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa ambapo pia mgogoro wa Misri umezingatiwa.

Msemaji wa kamisheni ya Umoja wa Afrika bwana Nouredine Mezni amearifu kuwa jopo hilo la marais watano litaongozwa na rais wa Mauretania Ould Abdel Aziz ambae pia ni mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

Marais hao ikiwa pamoja na Jakaya Kikwete wa Tanzania wamepewa muda wa mwezi mmoja kutafuta suluhisho la mgogoro wa Ivory Coast. Marais wengine ni Jacob Zuma wa Afrika kusini, Campaore wa Burkina Faso na Idriss Deby wa Chad.

Mgogoro huo ulitokea baada ya rais Gbagbo aliepo madarakani kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi, ingawa hesabu za kura zilionyesha hapo awali kuwa kiongozi wa upinzani Alassane Outtara ndiye aliekuwa mshindi halali.Jumuiya ya kimataifa inamtambua Outtara kuwa mshindi na rais wa Ivory Coast .

Katika muda wa mwezi mmoja jopo la marais hao linatarajiwa kufikia maamuzi yatakayokuwa na nguvu za kisheria.

Kwenye kikao chao cha siku mbili mjini Addis Ababa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika pia wamejadili matukio ya Misri na Tunisia.

Akihutubia kwenye kikao hicho leo mjini Addis Ababa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliunga mkono hatua ya Umoja wa Afrika ya kuliunda jopo litakaloushughulikia mgogoro wa kisiasa nchini Ivory Coast.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu Ban pia aliahidi kuwa Umoja wa Mataifa utasimama pamoja na Umoja wa Afrika katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Ivory Coast.Amesema Umoja wa Mataifa upo tayari kushirikiana na jopo la Umoja wa Afrika kwa undani, kwa kadri itakavyowezekana.

Katibu mkuu huyo pia aliwakumbusha viongozi wa nchi za Afrika juu ya umuhimu mkubwa wa changamato zinazoikabili Sudan baada ya watu wa Sudan ya Kusini kupiga kura ya kuamua kujitenga na Sudan ya Kaskazini.Katibu Mkuu Ban Ki-moon pia amesisitiza juu ya umuhimu wa Somalia- ambayo bado imo katika harakati za kuwania kuunda serikali .

Naye Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping amesema kuwa serikali ya mpito ya Somalia imeshindwa kufikia shabaha zake, lakini ametao mwito wa kuiunga mkono zaidi serikali hiyo.

Juu ya Sudan ,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa jambo muhimu sasa ni kwa pande zote zinazohusika kuanzisha juhudi za haraka ili kuyatatua matatizo yote yanayofuatia kura ya maoni.

Kwenye kikao chao kinachomalizika leo mjini Addis Ababa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika pia wamelijadili jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFP/Schadomsky/

Mhariri/ Abdul-Rahman.