1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Umoja wa Afrika kuanzisha mchakato wa maridhiano Libya

20 Februari 2023

Umoja wa Afrika umesema unaratibu mkutano a maridhiano ya kitaifa kwa ajili ya Libya, ikiwa ni jaribio la mwisho la kurejesha hali ya utulivu katika taifa hilo lililoharibiwa na vita.

https://p.dw.com/p/4NifD
Äthiopien | African Union Gipfel in Addis Ababa | Gruppenbild
Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Tamko hili la kuanzishwa kwa mchakato wa kusaka maridhiano nchini Libya, limetolewa katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa Umoja huo uliofanyika makao yake makuu, Addis Ababa, Ethiopia. 

Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameliambia shirika la habari la AFP katika siku ya mwisho ya mkutano huo wa kilele jana Jumapili kwamba, wamefanikiwa kukutana na pande tofauti tofauti, na sasa wapo katika mchakato wa kushirikiana nao kuhusiana na maandalizi ya siku na mahali patakapofanyika mkutano huo.

Mahamat amesema, mkutano huo utaongozwa na mpatanishi mkuu wa umoja huo nchini Libya, ambaye ni rais wa Jamhuri ya Kongo, Denis Sassou Nguesso.

Soma Zaidi: Kizungumkuti cha serikali mpya nchini Libya

Libya imejikuta katika mzozo tangu mwaka 2011, baada ya kuangushwa kwa utawala wa Moamer Kadhafi, katika uasi ulioungwa mkono na wanajeshi wa jumuiya ya kujihami ya NATO. Tangu mwezi Machi mwaka jana, serikali ya Libya ya upande wa mashariki inayoongozwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar mwenye mahusiano ya karibu na Urusi na Misri imekuwa ikiishutumu serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, inayoongozwa na waziri mkuu Abdullamid Dbeibah, ikidai imepitisha muda wake mamlakani.

Soma Zaidi:UN yahimiza pande pinzani Libya kukubaliana kuhusu uchaguzi

Mapema mwezi huu, Umoja wa mataifa ulitangaza kwamba maafisa waandamizi kutoka serikali hizo zinazokinzana wameanzisha utaratibu wa kuwaondoa wanajeshi wa kigeni pamoja na mamluki. Hata hivyo, mjadala ulioongozwa na mjumbe wa Umoja huo Abdoulaye Bathily ulishindwa kuandaa ratiba ama hatua madhubuti za kuondolewa kwa wanajeshi hao, waliotarajiwa kufikia 20,000 mwaka 2021, kulingana na Umoja huo.  

Burkina Faso | PK Ibrahim Traore
Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso kapteni Ibrahim Traore baada ya kutwa madaraka kwa njia ya mapinduzi Oktoba, 2022Picha: AA/picture alliance

Umoja wa Afrika wasisitiza hautakubaliana na njia zisizofuata katiba kujipatia madaraka. 

Mbali na Libya, Umoja huo pia umezungumzia sera yake ya kutokuvumilia kabisa mabadiliko yasiyo ya kikatiba, huku ikisema itaendelea kuyasimmaisha mataifa yanayoongozwa na tawala za kijeshi. Mataifa ya ukanda wa Sahel ya Burkina Faso, Guinea na Mali pamoja na Sudan yalisimamishwa uanachama kwenye umoja huo kufuatia mapinduzi ya miaka ya karibuni, ingawa, kamishna wa mahusiano ya siasa, amani na usalama wa umoja huo Bankole Adeoye aliashiria utayari wa kuyasaidia kurejea kwenye utawala wa kidemokrasia.

"Halmashauri iko tayari kuyasaidia mataifa wanachama kurejea kwenye utaratibu wa kikatiba. Cha muhimu ni kwamba demokrasia inatakiwa kuchukua mkondo wake, inatakiwa kupiganiwa na kulindwa," alisema Adeoye.

Katika hatua nyingine, rais wa Kenya William Ruto ametoa mwito kwa mataifa tajiri kuwajibishwa kwa kuchochea ongezeko la joto ulimwenguni na mabadiliko kwenye taasisi za kifedha za kimataifa kama miongoni mwa hatua za kukabiliana vema na mabadiliko ya tabianchi, suala ambalo pia limeugubika mkutano huo. Amesema hayo pembezoni mwa mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Amesisitiza kwamba mataifa masikini na hususan ya Afrika yamekumbwa na athari kubwa za mabadiliko hayo na kuchochea ukame na mafuriko licha ya kuchangia kidogo kwenye uzalishaji wa gesi ukaa.