1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kutumia majeshi kuzuwia wahamiaji

Admin.WagnerD3 Desemba 2013

Umoja wa Ulaya unatafakari uwezekano wa kushirikisha vikosi vya wanajeshi kusini mwa bahari ya Mediterranean katika juhudi za kuzuwia wahamiaji haramu na wakimbizi kuingia barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1ASQE
Picha: Sakis Mitrolidis/AFP/Getty Images

Wazo la kuendesha operesheni za kijeshi lilitolewa kwa mara ya kwanza katika pendekezo la Italia la Oktoba 24, lililotaka hatua kali zichuliwe baada ya matukio yaliyosababisha maafa makubwa katika kisiwa cha Lampedusa, jimboni Sicily, ambako boti iliyoondokea nchini Libya Oktoba 3, ilizama kabla ya kutia nanga kisiwani hapo na kuwauwa wahamaiaji wapatao 360.

Wakimbizi wakielekea kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.
Wakimbizi wakielekea kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.Picha: Reuters

Tukio hilo lililishtua bara la Ulaya na kuibua mjadala wa kiraia kuhusu gharama za kibinaadamu zinazosababishwa na sera ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya. Lakini viongozi wengi wa umoja huo wameuchukulia mkasa huo kama sababu ya kuongeza shughuli za kijeshi katika kanda hiyo.

Sera ya usalama na ulinzi, CSDP
Naibu msemaji wa idara ya huduma za hatua za nje ya Umoja wa Ulaya, EEAS, Sebastien Brabant aliliambia shirika la habari la IPS katika mahojiano baada ya tukio la Lampedusa, kwamba kikosi kazi cha Mediterranean kiliundwa ili kuja na mapendekezo ya hatua za mara moja kutoka kwa Umoja wa Ulaya, ambayo yamezaa sera ya pamoja ya usalama na ulinzi CSDP.

Pendekezo hilo linajumuisha njia za kuzuwia mienendo ya watu kuelekea barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa operesheni huru ya baharini, au utekekelezaji wa hatua za ziada ndani ya operesheni za wakala wa usimamizi wa mipaka wa umoja wa Ulaya, Frontex katika kanda hiyo.

Njia zote zinabashiri jukumu la sera ya CSDP, zana muhimu ya kushughulikia migogoro ya kimataifa ya kiusalama. Pendekezo la CSDP kama jukwaa la kushughulikia mienendo ya ya watu inayoweza kutokana na kuyavuruga mataifa ya Mediterranean limekuja wakati ukisubiriwa uamuzi kuhusu mustkabali wa chombo hicho katika ajenda ya mkutano wa baraza la Ulaya, unaopangwa kufanyika baadae mwezi huu.

Wakimbizi waliohamia nchini Ugiriki.
Wakimbizi waliohamia nchini Ugiriki.Picha: Reuters

Upinzani dhidi ya CSDP
Idara ya huduma za hatua za nje ya Umoja wa Ulaya, EEAS itawasilisha pendekezo wakati wakuu wa nchi wakijadili namna ya kuboresha uwezo wa kiulinzi, kuimarisha sekta ya ulinzi na kuboresha ufanisi, muonekano na athari za CSDP.

Hata hivyo, wazo hilo limekumbana na upinzani, ambapo mbunge kutoka Ujerumani Andrej Hunko, mjumbe wa mkutano wa bunge la baraza la Ulaya, alisema kuongeza shughuli za kijeshi katika uchunguzi wa mipaka kutafanya uvukaji wa mipaka kuwa wa hatari zaidi na hata kusababisha vifo zaidi, na kuongeza kuwa hata EEAS inathibisha hili. Anasema njia zisizo na kiutu zinazotumiwa na polisi ya mipaka ya Umoja wa Ulaya, Frontex zinazidi kuimarishwa.

Kuweka shughuli za kijeshi katikati mwa bahari ya Mediterranean kutashadidia vikwazo vya awali vilivyowekwa katika eneo la kusini-mashariki mwa bahari hiyo. Mwaka 2012, Ugiriki ilianzisha sera kali, zikiwemo kuweka vikosi vya usalama katika mipaka yake, kujenga ukuta katika mpaka wake na Uturuki, na kuwaweka kizuizini wahamiaji haramu kwa hadi miezi 18.

Askari wakilinda doria katika bahari ya mediterranean.
Askari wakilinda doria katika bahari ya mediterranean.Picha: picture-alliance/dpa

Wahamiaji nao wazidi kuchemsha bongo
Matokeo ya hatua hizo yalikuwa ni kuanzishwa kwa njia mpya kupitia magharibi mwa mataifa ya Balkan, au kuhuisha njia za zamani nchini Misri, Libya na Tunisia. Wakati huo huo, Uhispania ilianzisha mradi wa udhibiti wa mipaka CLOSEYE, wenye gharama ya mamilioni, ambao utapelekea kuwekwa kwa ndege za uchunguzi kusini-magharibi mwa bahari ya Mediterranean.

Martin Lemberg-Pedersen, profesa msaidizi katika kituo cha masomo ya uhamiaji katika chuo kikuu cha Copenhagen anasema mapendekezo ya EEAS yamewasilishwa wakati ambapo mfumo wa uchunguzi wa mipaka wa Umoja wa Ulaya, EUROSUR, unakaribia kuanza kazi. Mfumo huu ambao umeundwa kwa ushirikiano w akaribu na sekta ya silaha ya ulaya, unasisitiza malengo sawa kabisaa na yale yaliyobainishwa katika njia za EEAS.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ips
Mhariri: Saum Yusuf