1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukatili unafanywa na pande zote za mgogoro Cameroon: Amnesty

4 Julai 2023

Shirika la kimataifa la Amnesty International limesema kuwa vikosi vya usalama, waasi wanaopigania kujitenga na wapiganaji wa kikabila wamefanya "ukatili" katika eneo lenye machafuko nchini Cameroon.

https://p.dw.com/p/4TNtB
Symbolbild I Cameroon anglophone rebel
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Uovu huo ni pamoja na watu kunyongwa, kuteswa na kubakwa. Ripoti yake imegundua ushahidi mpya wa ukiukaji katika eneo la Kaskazini magharibi, moja kati ya majimbo mawili ya magharibi ambako wanamgambo wanaotumia kiingereza walitangaza uhuru kutoka kwa taifa hilo ambalo idadi kubwa wanazungumza Kifaransa.

Tamko lao, ambalo halijawahi kutambuliwa kimataifa, lilichochea msako wa serikali ya mjini Yaounde. Ripoti ya Amnesty International imesema raia hujikuta katika mgogoro kati ya jeshi, waasi wanaotaka kujitenga na wanamgambo.

Watu wa jamii ya Mbororo Fulani wamekuwa wakilengwa na waasi wanaotaka kujitenga, kwa sehemu kwa sababu wanazingatiwa kuwa wanaiunga mkono serikali iliyoko madarakani.

Hali ilipozidi kuwa mbaya, wanamgambo wengi wao kutoka jamii ya Mbororo Fulani, wakiungwa mkono au kuvumiliwa na serikali, wamefanya unyanyasaji dhidi ya wakaazi.