1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa kulinda amani Darfur wamalizika rasmi

Daniel Gakuba
31 Desemba 2020

Ujumbe wa amani wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika jimbo la Darfur nchini Sudan - UNAMID unamalizika rasmi Desemba 31 2020 baada ya kuwepo kwa miaka 13.

https://p.dw.com/p/3nPYr
UNAMID Mission in Darfur, Sudan
Picha: AFP via Getty Images

Ujumbe huo wa kijeshi ulipelekwa mwaka 2003, baada ya mapigano makali kuibuka baina ya waasi kutoka makabila ya watu weusi na serikali ya mjini Khartoum inayodhibitiwa na Waarabu. Serikali hiyo iliukandamiza uasi huo kwa nguvu kubwa, ikitumia wanamgambo wa Kiarabu waliojulikana kama Janjaweed.

Watu wapatao 300,000 waliuawa katika ghasia hizo, na wengine zaidi ya milioni 2.5 walipoteza makaazi yao, hii ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Soma zaidi: Ujumbe wa UNAMID wapendekezwa kuondolewa Darfur

Taarifa ya UNAMID iliyochapishwa jana Jumatano ilisema, ''Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika jimboni Darfur utahitimisha operesheni zake siku ya Alhamis, baada ya serikali ya Sudan kuchukua majukumu ya kuwalinda raia wa jimbo hilo.''

Hali ya afueni iliyodumu kwa muda

Kwa sehemu kubwa, uhasama katika jimbo la Darfur umepungua mnamo miaka ya karibuni, na utawala wa kiimla wa muda mrefu wa Rais Omar al-Bashir anayetafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na uhalifu mwingine, uliangushwa Aprili, 2019.

Hata hivyo, serikali ya mpito inayoiongoza Sudan bado ni dhaifu, na makabiliano ya kikabila yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara jimboni Darfur, yakiwemo ya wiki iliyopita ambamo watu 15 waliuawa na wengine dazeni kadhaa wakajeruhiwa.

Wenyeji wa Darfur, wengi wao wakiwa wameishi kwa muda mrefu katika kambi zilizofurika, wamefanya maandamano kwa wiki kadhaa zilizopita, wakipinga kuondolewa kwa ujumbe wa UNAMID.

Sudan Darfur UN Mission UNAMID
Darfur imeshuhudia machafuko tangu 2003Picha: picture-alliance/AP Photo/UNAMID/A. G. Farran

''Maisha ya watu wa Darfur yako hatarini, Umoja wa Mataifa hauna budi kutafakari upya uamuzi wake,''  alisema Mohammed Abdulrahman, mkimbizi katika kambi ya Kalma kwenye mji wa Nyala, makao makuu ya jimbo la Darfur Kusini.

Yeye ni mmoja wa wakimbizi mamia kadhaa walioandamana na kukita kambi nje ya makao makuu ya UNAMID.

Wasiwasi wa usalama miongoni mwa wakaazi 

Waandamanaji hao walikuwa na bango lenye ujumbe usemao: ''Tuna imani katika ulinzi wa Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi wa ndani,'' na ''Tunapinga kuondolewa kwa ujumbe wa UNAMID.''

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waanzisha ujumbe wa kisiasa kusaidia Sudan

Umoja wa Mataifa umesema maafisa wake wapatao 8,000, wakiwemo wa kijeshi na wa kiraia, wataanza kuondoka hatua kwa hatua kuanzia mwezi Januari, na kukamilisha mchakato huo kwa kipindi cha miezi sita.

Mkazi mwingine wa muda mrefu wa kambi ya Kalma, Othman Abulkassem anahofia kuwa kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kunaashiria matatizo kwa watu wa Darfur. Lakini, msemaji wa UNAMID Ashraf Eissa amejaribu kutuliza hofu hiyo ya watu wa Darfur.

Umoja wa Mataifa watuliza hofu

''Tunaelewa wasiwasi wa wakaazi wa Darfur, hususan wale ambao ni wakimbizi wa ndani, na wale kutoka makundi mengine dhaifu. Lakini hali imeboreka kwa kiasi kikubwa mnamo miaka michache iliyopita,'' alisema Eissa katika mahojiano na shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa, ''Hivi sasa ni wajibu wa serikali ya Sudan na watu wake kuhakikisha usalama wao wenyewe jimboni Darfur.''

Nafasi ya UNAMID itachukuliwa ujumbe mwingine wa Umoja wa Mataifa utakaosimamia kipindi cha mpito nchini Sudan (UNITAMS). Ujumbe huo mpya utakuwa na jukumu la kuisaidia serikali ya Sudan katika mchakato huo, kuimarisha amani na kuusambaza msaada kwa wenye mahitaji.

AFP, DPA, Reuters, AP