1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Marekani wawasili Kenya kuzungumzia uchaguzi

18 Agosti 2022

Ujumbe wa bunge la Marekani umewasili nchini Kenya kukutana na rais mpya mteule na kiongozi wa upinzani anaetafakari kufungua kesi kupinga matokeo katika mzozo wa karibuni wa uchaguzi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4FiBi
Nairobi | US-Kongressdelegation in Kenia inmitten einer Wahlkrise
Picha: Shisia Wasilwa

Balozi mpya wa Marekani nchini Kenya, Meg Whitman, alisema ujumbe unaoongozwa na Seneta Chris Coons pia utakutana na Rais wa Kenya anayeondoka Uhuru Kenyatta, ambaye amekuwa kimya hadharani tangu uchaguzi wa Agosti 9 ambao kwa kiasi kikubwa ulifanyika kwa amani.

Rais mteule William Ruto ndiye naibu rais wa Kenyatta, lakini wawili hao walitofautiana miaka iliyopita, na Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka huu alimuunga mkono kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga badala yake.

Soma pia: Maoni: Uchaguzi wa Kenya 2022 wathibitisha mageuzi bado yanahitajika

Odinga amesema anaangalia "njia zote za kikatiba na kisheria'' ili kupinga kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu. Kampeni yake imesalia na wiki moja kutoka tangazo la Jumatatu la ushindi wa Ruto kwenda katika Mahakama ya Juu, ambayo pia itakuwa na siku 14 kutoa uamuzi. Odinga amewataka wafuasi wake kuwa watulivu katika nchi yenye historia ya ghasia za baada ya uchaguzi.

Kenia Thika | William Ruto während Wahllkampfveranstaltung
Tume ya Uchaguzi Kenya, IEBC, ilimtangaza William Ruto kuwa rais mpya mteule, akimshinda Raila Odinga, alieungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta.Picha: Ed Ram/Getty Images

Tume ya uchaguzi nchini Kenya iligawanyika hadharani na kushuhudiwa machafuko dakika chache kabla ya tangazo hilo la Jumatatu, huku makamishna wakishutumiana kwa utovu wa nidhamu. Makamishna wanne waliopinga tamko hilo la Jumatatu waliteuliwa na Kenyatta mwaka jana.

Mgawanyiko huo ulikua mshtuko kwa Wakenya wengi baada ya uchaguzi ulioonekana kuwa na uwazi zaidi kuwahi kutokea nchini humo, huku matokeo kutoka vituo zaidi ya 46,000 yakichapishwa mtandaoni kwa umma kuyafuatilia. Hesabu za umma, ikiwa ni pamoja na kundi moja la waangalizi wa eneo la uchaguzi, zilithibitisha ushindi wa Ruto kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Soma pia: Ruto: Kutoka mpwaguzi hadi rais aliechaguliwa Kenya

Mabadiliko ya kisiasa nchini Kenya yatakuwa na athari kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo Kenyatta alikuwa akifanya kazi na Marekani kujaribu kupatanisha mgogoro wa Ethiopia wa Tigray na kuendeleza juhudi za amani kati ya Rwanda na Kongo. Ruto katika maoni yake kwa umma wiki hii ameangazia maswala ya nyumbani, sio ya kikanda.

Coons, mjumbe wa Kamati ya Seneti kuhusu Mahusiano ya Kigeni, na wajumbe wake tayari wametembelea Cape Verde na Msumbiji na wanatarajiwa kuzuru Rwanda, ambapo mvutano wa Kongo na haki za binadamu unapaswa kuwa ajenda kufuatia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken mjini Kigali wiki iliyopita.

Kenia Nairobi | Raila Odinga und Unterstützer
Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga, akiwasili kabla ya kutoa hotuba kwa taifa kwenye makao makuu ya kampeni yake mjini Nairobi, Agosti 16, 2022.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Ruto mwenye umri wa miaka 55 aliwashawishi Wakenya kwa kuugeuza uchaguzi huo kuhusu tofauti za kiuchumi na sio zile za kikabila ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikigubika siasa za nchi hiyo na kusababisha matokeo mabaya wakati mwingine. Alijionyesha kama mtu wa nje mwenye mwanzo wa umaskini na anaepinga himaya za kisiasa za Kenyatta na Odinga, ambao baba zao walikuwa rais wa kwanza wa Kenya na makamu wa rais mtawalia.

Odinga mwenye umri wa miaka 77 amewania kiti cha urais kwa robo karne. Anajulikana kama mpiganaji na alifungwa mnamo miaka ya 1980 kutokana na msukumo wake wa kudai demokrasia ya vyama vingi. Pia alikuwa mfuasi wa katiba ya mwaka wa 2010 ya Kenya.

Chanzo: APE