Ujerumani yaonya juu ya "vita vya mawakala" Iraq
15 Juni 2014Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier Jumapili (15.06.2014) ameonya kwamba mzozo wa umwagaji damu unaoendelea nchini Iraq unaweza kubadilika kwa haraka na kuwa vita vya mawakala watakaopigana kuyawakilisha mataifa makubwa.
Akizungumza na gazeti la Ujerumani la Jumapili "Welt am Sonntag" ametowa wito kwa Uturuki,Mataifa ya Kiarabu ya Ghuba na Iran kutimiza wajibu wao katika kuleta utulivu nchini Iraq.
Amekaririwa akisema "Inabidi tuzuwiye kuzuka kwa vita vya mataifa yatakayowakilishwa vitani na mawakala wao katika ardhi ya Iraq."
Steinmeier amesema mataifa yaliko katika kanda hiyo hayawezi kuwa na manufaa kwa kuwa na eneo linalotanuka ziada ya Syria kwenye uwa wao kama mahala pa kufanyia maovu kwa makundi ya mamluki, Waislamu wa itikadi kali wa kila aina na magaidi.
Amefuta uwezekano wa Ujerumani kujihusisha kijeshi katika mzozo huo na kutamka wazi kwa mara nyengine tena kwamba ni wajibu wa jeshi la ulinzi la Iraq kuwazuwiya wapiganaji hao wa itikadi kali za Kiislamu.
Serikali yakosolewa
Steinmeier pia ameikosowa serikali ya Iraq kwa kushindwa kuwajumuisha katika serikali ya nchi hiyo makundi hasimu ya kanda,kikabila na kidini.
Ameongeza kusema msaada wa kimataifa haukutumiwa kwa ufanisi katika kuleta hali ya utulivu wa kisiasa na kiuchumi nchini humo ambapo Ujerumani imetowa kama euro milioni 400 katika msaada kwa Iraq katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameliambia gazeti hilo kwamba Ujerumani ipo tayari kushiriki kwa kiwango kidogo katika juhudi za kuimarisha Iraq lakini amesema hawezi kufikiria mazingira ambapo kwayo wanajeshi wa Ujerumani wanaweza kutumika nchini humo.
Waziri huyo aliwahi kusema hivi karibuni mjini Berlin kwamba hakuna "muarubaini" wa kutibu mara moja mzozo huo unaozidi kukuwa nchini Iraq na kwamba kulizuwiya kundi la wapiganaji la Dola la Kiislamu la Iraq na Sham (ISIL) kunahitaji serikali ambayo inaweza kutumia nguvu za mamlaka yake katika nchi yake.
Wananchi wamejitolea kwa kujiunga na jeshi kuitikia wito wa Kiongozi Mkuu wa Kidini nchini humo wa madhehebu ya Shia mwenye ushawishi Ayatollah Ali al- Sistani wa kuchukuwa silaha kuzuwiya kusonga mbele kwa wapiganaji hao wa madhehebu ya Sunni wa itikadi kali ambao wanasonga mbele kuelekea mji mkuu wa Baghdad baada ya kuuteka mji wa pili kwa ukubwa nchini humo Mosul .
Iran yaonya
Iran imeonya hapo Jumapili dhidi ya kuchukuliwa kwa hatua yoyote ya kuingilia kijeshi nchini Iraq. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Marzieh Afkham amesema mjini Tehran ana imani kwamba serikali na wananchi wa Iraq wataweza kuzima njama hiyo na nchi hiyo ina uwezo na maandalizi yanayohitajika ya kupambana na ugaidi na misimamo mikali ya kidini.
Amesema kuingilia kati kijeshi kutauzidisha tu mzozo huo.Kauli yake hiyo inakuja wakati Marekani ikitangaza kwamba inatuma meli zake za kivita katika eneo la Ghuba.
Hapo Jumamosi Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema anaamini kwamba wananchi wa Iraq wana uwezo wa kuzima ugaidi na kwamba Iran haikuombwa kusaidia na nchi hiyo jirani.
Serikali ya Iraq Jumapili imeanza kujibu mashambulizi ya wanamgambo hao ambapo makamanda wake wamesema hivi sasa wameanza kuwarudisha nyuma wanamgambo hao na kwamba wanajeshi wameikombowa miji miwili kaskazini mwa Baghdad.
Wanajeshi hao wanatazamiwa kuungana na mamia ya wananchi wa kujitolea walioitikia wito wa Kiongozi Mkuu wa Kidini nchini humo Ayatollah Ali al-Sistani.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/dpa/rtr
Mhariri : Caro Robi