1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaitimua nje Argentina 4:0

3 Julai 2010

Je,Maradona atamfuata dunga wa Brazil ?

https://p.dw.com/p/OA4Q
Kikosi cha Ujerumani kilichoitumua Argentina 4:0Picha: AP

UJERUMANI 4:ARGENTINA 0

Ujerumani, imeichezesha leo Argentina, kindumbwe-ndumbwe charira na kuiabisha kwa mabao 4:0 ili kujiunga na Holland na Uruguay duru ijayo. Ilikua siku ya Miroslav Klose na Schweinsteiger kutamba na halkadhalika Mueller.

Ujerumani, ilitangulia tayari mnamo dakika ya 3 ya mchezo pale mkwaju wa (free-kick ) alioupiga Schweinsteiger, kumkuta Mueller,alieusindikiza kwa kichwa katika lango la Argentina.Ujerumani ikidhibiti mchezo, ilichukua hadi dakkika ya 22 ya mchezo pale Tavez kupioga hodi katika lango la Ujerumani ,lakini kipa Neuer hakumkaribisha ndani.

Dakkka 1 tu baadae,Mueller kutoka wingi wa kulia alitoa pasi maridadi ajabu kwa Klose,lakini mkwaju wake ulipaa juu.Dakika 36 ya mchezo,Higuain,alilifumania lango la Ujerumani,lakini aliotea.Ujerumani ikatia bao la pili pale Klose alipopewa pasi maridadi karibu na chaki ya lango la argentina na mara hii hakukosea. Argentina, ikijitahidi kufuta mabao hayo 2 ya Ujerumani, mlinzi Ernie Friederich aliipatia Ujerumani bao la 3 kufuatia pasi maridadi ya Schweinsteiger,ambae leo ndie ufungo wa ushindi wa Ujerumani. Miroslav Klose, akaupiga msumari wa mwisho katika lango la Argentina na kuifungisha virago kurudi Buenos Aires na mabao 4 kama Australia na Uingereza.

Ujerumani na Argentina zikiania kuamua nani kati yao ataifuata Holland na Uruguay, katika nusu-finali baada ya Holland jana kuwatimua nje mabingwa mara 5 wa dunia - Brazil; na Uruguay kuwatia kitanzi Black Stars-Ghana na kuzusha msiba mkubwa sio tu Accra ,bali Afrika nzima kutoka Johannesberg hadi Accra, Abuja hadi Dar-es-salaam.

Huku Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani ,aliefika binafsi uwanjani Cape Town akiwa ubavuni mwa Rais Zuma, kuwatia shime watoto wake na kumpa pongezi Rais Zuma kwa maandalio mazuri ya Kombe hili la dunia , alibainisha amewasili na baraka njema kutoka Ujerumani.Dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, Argentina ilichachamaa sana kusawazisha bao la mapema la Ujerumani. Hata Mueller alikosea bao dakika kabla firimbi ya mapumziko.

Tangu mapema asubuhi ya leo,maalfu ya mashabiki wa Ujerumani,wake kwa waume,wakubwa kwa wadogo, wamepiga kambi vituo mbali mbali wakishangiria ushindi dhidi ya Gaucho.Nini hatima ya kocha Diego Maradona na je atafuata mkondo wa kocha wa Brazil.Dunga na kun'gatuka ?

Kabla firimbi kulia kuanzisha changamoto hii kati ya Ujerumani na Argentina, kocha wa Ujerumani Joachim Löw,alisema:

"Sote tunajua kwamba, tuna uwezo wa kusonga mbele na tuna nia ya kufika mbali zaidi.Sasa tumo katika kundi la timu 8 za mwisho na shabaha yetu ni kuwa miongoni mwa timu 4 za mwisho."

Holland iliioipiga jana kumbo Brazil kwa mabao 2-1 na Uruguay, ilioitia kitanzi Black Stars-Ghana, zimeweka miadi ya nusu-finali ya kwanza . Wesley Sneijder, ndie aliekuwa nyota ya rangi ya chungwa kwa wadachi wakati Felipe Melo, ndie alieichimbia kaburi na kuizika Brazil -timu yake hapo jana.Ni Snieder alieupiga mkwaju ili Melo ausindikize kwa kichwa katika lango lake na Holland kusawazisha bao 1:1 huko Port Elizabeth.

Ilikua Brazil lakini, iliotangulia kwa bao dakika ya 10 ya mchezo pale Melo huyo huyo alipompasia dimba maridadi ajabu Robino nae akalifumania lango la Holland. Baada ya bao la pili la Sneider kwa kichwa, Melo aliingiwa na wazimu na akamtimba vibaya sana stadi wa Holland Arjen Robben.Hapo rifu akamtimua nje ya uwanja na samba huko Copa Cabana Brazil ghafula ikazimika.

Akiueleza mchezo ulivyokwenda,mlinzi wa kati wa Holland,anaeichezea Bayern Munich:Mark van Bommel alisema.

"Haukua mchezo wa kuvutia, tena kwa pande zote mbili.Vilikuwa vita vikali uwanjani.Kipindi cha kwanza,mara kwa mara , tukichelewa hatua 1 na halafu tukafungwa bao kutoka kati ya uwanja na hili ni kosa kubwa kutokea hivyo.

Na baada ya sare ya bao 1:1 ambayo ilikua kama bahati tu,tulipiga kuona ilioongoza bao la pili na kufanya matokeo 2:1.Mwishoe, kila mmmoja alitokwa na jasho."

Alisema van Bommel.

Uruguay, imewasili nusu-finali yake ya kwanza tangu kupita miaka 40 kwa kuitia kitanzi Ghana, tumaini la mwisho la Afrika katika Kombe hili la Dunia 2010.

Ghana ikiania kuwa timu ya kwanza kabisa ya Afrika kuwasili nusu-fianli ya Kombe hili baada ya Kameroun 1990 na Senegal, 2002 kuwasili hatua hii ya robo-finali.Na Ghana, ilikuwa sekunde tu mbali na nusu-finali ilipozimwa.

Leo usiku tutajua iwapo ni mabingwa wa Ulaya, Spain au Paraguay ,watajiunga na Holland ,Uruguay na Ujerumani katika duru ya nusu-finali. Spain, ikitamba na David Villa, inaamini leo usiku ni zamu ya gombe-dume lao, Torres, kuwika na kuthibitisha waliosema wapiga-ramli kuwa "huu ni mwaka wa Spain" kuvaa taji la dunia.Wadachi na Wajerumani wana ajenda nyengine.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Mohamed Dahman