1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Ujerumani, Ufaransa wataka usaidizi wa Afrika dhidi ya Putin

13 Januari 2023

Mawaziri wa Ujerumani na Ufaransa wametoa wito wa kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika katika kukabiliana na mizozo ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4M9ko
Außenministerin Baerbock in Äthiopien
Picha: picture alliance/dpa

Wakizungumza Ijumaa na viongozi wa Umoja wa Afrika katika makao makuu ya umoja huo ulioko kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, wanadiplomasia hao wamesema Ujerumani na Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya zinategemea kuungwa mkono na Afrika, katika kukabiliana na mizozo ulimwenguni, ikiwemo uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa chakula.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesema wao kama watu wa Ulaya wanahitaji kuungwa mkono na washirika wao ulimwenguni kote katika wakati ambapo amani ya Ulaya imeshambuliwa kwa vita vya kichokozi vya Urusi.

Afrika iunge mkono mageuzi ya Umoja wa Mataifa

Aidha, ameutaka Umoja wa Afrika kuunga mkono mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yataongeza viti vingine vya kudumu kwenye chombo hicho, ikiwemo viwili kwa ajili ya Afrika.

 ''Kwa hivyo, tunaunga mkono viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama pia kwa bara la Afrika, na ili kuzidisha ushirikiano wetu ni muhimu tufanye kazi pamoja kati ya nchi mbili, lakini pia uhusiano wa bara na bara kwa jina la watu wetu ni muhimu," alisema Bearbock.

Äthiopien Adama | Getreidelager UN-Welternährungsprogramm | Annalena Baerbock & Catherine Colonna
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Annalena Baerbock wakilitembelea ghala la nafaka la Umoja wa MataifaPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Baerbock amesema nchi za Ulaya na Afrika ni majirani sio tu kijiografia, lakini pia katika mioyo yao. Mwanadiplomasia huyo wa juu wa Ujerumani, alikuwa akizungumza sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat.

Colonna pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pande nyingi na umuhimu wa mageuzi katika Umoja wa Mataifa. Waziri huyo wa Ufaransa amesema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unatishia kanuni za msingi zilizoainishwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Ushirikiano dhidi ya ugaidi

Pia amezungumzia ushirikiano wa muda mrefu kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika nchini Somalia, pamoja na juhudi za Ufaransa na Ujerumani katika kukabiliana na ghasia na ugaidi kwenye ukanda wa Sahel.

Colonna amesema huo ni "ukosefu wa haki" kwamba Afrika haina uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ingawa asilimia 70 ya kazi za Baraza la Usalama zinahusiana na bara hilo.

Mapema wiki hii, Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang alijizuia kuzungumzia wito mpya uliotolewa na Umoja wa Afrika wa kutaka uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakati wa ziara yake nchini Ethiopia.

(DPA)