1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yawarai raia wake kuondoka Lebanon

30 Julai 2024

Uingereza imewatolea mwito raia wake kuondoka Lebanon na kutosafiri kwenda nchini humo katika wakati mivutano inazidi kutanuka kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4ispD
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza | David Lammy
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza David LammyPicha: Maja Smiejkowska/REUTERS

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza David Lammy amesema hali inabadilika haraka kwenye kanda hiyo na wizara yake inafanya kile iwezalo kuhakikisha usalama wa raia wa nchi hiyo.

Juhudi kubwa za kidiplomasia zinaendelea hivi sasa kutuliza joto la uhasama na kuzuia kuzuka vita kamili kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon wanaoungwa mkono na Iran.

Pande hizo mbili zimekuwa zikishambuliana karibu kila siku tangu kuzuka kwa vita vya Gaza lakini uhasama umefikia kiwango cha juu tangu kutokea shambulizi kwenye eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Milima ya Golan.

Israel inalituhumu kundi la Hezbollah kuhusika na shambulizi hilo la siku ya Jumamosi lililowaua vijana 12 na utawala mjini Tel Aviv umeapa kujibu kwa hatua kali.