1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yaiomba radhi Srebrenica kwa mauaji

11 Julai 2022

Uholanzi kwa mara ya kwanza imewaomba radhi watu wa Srebrenica baada ya miaka 27 tangu jeshi lake liliposhindwa kuwajibika kuzuia mauaji ya halaiki katika mji wa Srebrenica nchini Bosnia wakati wa vita vya Balkan.

https://p.dw.com/p/4DyJg
Jahrestag Massaker Srebrenica
Picha: Armin Durgut/AP/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Uholanzi Kasja Ollogren amesema wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji hayo katika kijiji cha Potocari kilichopo manispaa ya Srebrenica kwamba "Jumuiya ya kimataifa ilishindwa kutoa ulinzi unaofaa kwa watu wa Srebrenica. Serikali ya Uholanzi nayo inakiri kuwa miongoni mwa walioshindwa kuchukua jukumu dhidi ya hatua hiyo. Na ni kutokana na hali, tunaomba radhi sana."

Vita vya Balkan vilizuka miaka ya 1990, wakati iliyokuwa Yugoslavia iliposambaratika na hatimaye kuundwa mataifa mapya sita. Vita vibaya zaidi vikaibuka kati ya Bosnia-Herzegovina, wakati vikosi vya kikabila vya Serbia vilipopambana na Waislamu na vikosi vya kikabila vya Croatia juu ya udhibiti wa eneo hilo.

Katika majira ya joto ya 1995, vikosi vya Uholanzi chini ya kamandi ya Umoja wa Mataifa vilikuwa na jukumu la kuwalinda idadi kubwa wa watu waliokuwa waumini wa Kiislamu waliokuwa kwenye mji wa Srebrenica. Lakini hawakutoa upinzani wowote wakati vikosi vya kabila ya Serb chini ya uongozi wa Ratko Mladic vilipouvamia mji huo Julai 11.

Den Haag | Internationaler Strafgerichtshof | Ratko Mladic
Ratko Mladic akiwa mahakamani mjini The Hague, Juni 8, 2021 wakati alipokuwa akisomewa hukumu baada ya Umoja wa Mataifa kumkuta na hatia.Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Vikosi hivyo viliwaua karibu wanaume na wavulana 8,000 wa Kiislamu, katika kile kinachoonekana katika picha pana kama tukio baya kabisa la mauaji ya watu wengi barani Ulaya tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

Uholanzi ilishawahi kuzungumzia suala la kushindwa kisiasa, lakini haikuwahi kuomba radhi kwa uwazi kuhusiana na kushindwa kuwalinda raia hao.

Hata hivyo, Ollongren pia aliweka wazi kwamba mzigo wa lawama bado unabakia kwa majeshi yaliyofanya mauaji.

Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu wa kivita ilimkuta Mladic na hatia ya mauaji na kumuhukumu kifungo cha maisha jela, sambamba na Radovan Karadic, aliyekuwa kiongozi wa kisiasa wa vikosi vya Serbia.

Soma Zaidi: Miaka 25 baada ya Srebrenica, Mahakama kimataifa zahitajika

Kwenye maadhimisho hayo, masalia ya wahanga 50 pia yalizikwa. Kwenye eneo hilo la Potocari kuna makaburi 6,652. Wengine 237 walizikwa kwenye maeneo mengine, kufuatia maombi ya familia zao. Wahanga wengine 1,000 hawajulikani walipo hadi sasa.

Tizama Zaidi:

Srebrenica yawakumbuka wahanga wa mauaji

Mashirika: DPAE