1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yatupilia mbali mazungumzo na Catalonia

Daniel Gakuba
5 Oktoba 2017

Uhispania imekataa miito ya mazungumzo na mamlaka ya jimbo la Catalonia ambalo Jumapili liliendesha kura ya maoni yenye utata, ambayo viongozi wa jimbo hilo wanasema matokeo yanayowapa idhini ya kujitangazia uhuru

https://p.dw.com/p/2lFBj
Spanien Barcelona Streik für Unabhängigkeit
Viongozi wa jimbo la Catalonia wanatishia juu ya uwezekano wa kujitangazia uhuru wiki ijayoPicha: Getty Images/AFP/P.-P. Marcou

Wito wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili ulikuwa umetolewa na Umoja wa Ulaya, lakini mvutano umezidi kushamiri, baada ya kiongozi wa Catalonia, Carles Puigdemont kulaani uingiliaji kati wa mfalme wa Uhispania Felipe VI, na baada ya serikali mjini Madrid kutupilia mbali uwezekano wowote wa mazungumzo.

Tangazo la ofisi ya waziri mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy, limesema kwamba katika demokrasia ipo njia moja tu ya mazungumzo, nayo ni kufuata sheria. Ujumbe huo umesisitizwa katika kauli ya naibu waziri mkuu Soraya Saenz de Santamaria, aliyemshambulia vikali Puigdemont.

Spanien Regierungssprecherin Vizepräsidentin Soraya Saenz de Santamaria
Soraya Saenz de Santamaria, Naibu Waziri Mkuu wa UhispaniaPicha: dapd

De Santamaria amesema, ''Kila ujumbe unaotolewa na bwana Puigdemont ni mvutano mpya, na njia isiyoelekea kokote. Kwa sababu hakuna demokrasia nje ya sheria, hakuna haki nje ya sheria. Kwa muda mrefu bwana Puigdemont anaishi nje ya sheria, nje ya hali halisi, nje ya fikra sahihi''.

Catalonia kujitangazia uhuru wiki ijayo?

Huku viongozi wa Catalonia wakiendelea na shinikizo lao la kutaka kujitenga kutoka Uhispania, kiongozi wa jimbo hilo, Puigdemont, amesema sera za serikali ya Uhispania ni za hatari. Na katika kikao cha bunge la jimbo hilo jana, wabunge wanaounga mkono kujitenga wametaka kikao rasmi Jumatatu ijayo, kujadili matokeo ya kura ya Jumapili iliyopita.

Vyanzo kutoka ndani ya serikali ya jimbo hilo, vimelieleza shirika la habari la AFP kuwa kulingana na mwenendo ulivyo, yumkini Catalonia ikatangaza uhuru wake katika kikao hicho cha bunge.

Bila shaka hatua hiyo inaweza kuupeleka mzozo kati ya Catalonia na serikali kuu ya mjini Madrid katika hatua mbaya zaidi. Serikali hiyo, pamoja na mahakama, vinaichukulia kura ya maoni ya Jumapili kuwa kinyume cha sheria.

Siogopi kukamatwa na kufungwa: Puigdemont

Spanien Barcelona Carles Puigdemont
Carles Puigdemont, kinara wa harakati za kujitenga kwa CataloniaPicha: Reuters/A. Gea

Katika mahojiano yake na gazeti la Bild la Ujerumani, kiongozi wa Catalonia Puigdemont amesema hana hofu yoyote ya kuweza kukamatwa na kuwekwa jela. ''Siogopi tena kitu chochote kinachofanywa na serikali ya Uhispania'', amesema kiongozi huyo, akikiri kwamba uwezekano wa kufungwa upo.

Hata hivyo, ingawa serikali ya Uhispania imesema Puigdemont amevunja sheria, hakuna dhamira yoyote ya serikali hiyo, wala ya mahakama, iliyoelezwa kuhusiana na kumkamata, Puidemont.

Uchunguzi wa kura za maoni uliofanywa kabla ya kura ya Jumapili, ulionyesha kwamba asilimia 40 tu ya watu wa Catalonia, ndio wanaounga mkono jimbo hilo lenye mamlaka ya ndani kujitenga na Uhispania na kujitangaza kama Jamhuri huru.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga