1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania, Italia zatinga robo fainali UEFA Euro 2012

Admin.WagnerD19 Juni 2012

Kivumbi kilichotimka jana nchini Poland kwenye mechi za kundi C matokeo yake ni kwamba Uhispania na Italia zimefanikiwa kuingia robo fainali ya Uefa Euro 2012.

https://p.dw.com/p/15HUM
Spain's Jesus Navas scores his side's first goal during the Euro 2012 soccer championship Group C match between Croatia and Spain in Gdansk, Poland, Monday, June 18, 2012. (Foto:Gero Breloer/AP/dapd)
UEFA EURO 2012 Spanien Kroatien Jesus Navas TorPicha: AP

Mchezo baina ya Uhispania na Croatia ulikuwa wa vuta nikuvute ambapo kabla ya dakika ya 88 hakuna timu iliyokuwa mbabe wa mwenzake. Mambo yalibadilika baada ya Uhispania kumuingiza dimbani mchezaji wake Jesus Navas ambaye bila ajizi akaweka kimyani bao pekee la nchi hiyo na kuufanya mchezo huo kuwa 1-0.

Navas aliweza kuziona nyavu za wapinzani wake katika mchezo huo kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Cesc Fabrigas na Andres Iniesta katika dakika ya 88. Miongoni mwa patashika zitakazokumbukwa ni pamoja na ile ya mchezaji Ivan Rakitic wa Croatia na mlinda mlango wa Uhispania Iker Casillas mwendo wa dakika ya 58.

Kwa upande mwingine Italia nayo iliilazimisha Jamhuri ya Ireland kipigo cha bao 2-0 yakiwa ni matunda ya vijana machachari Antonio Cassano na Mario Balotelli.

Mashabiki wa Italia kwenye mechi za Uefa Euro 2012
Mashabiki wa Italia kwenye mechi za Uefa Euro 2012Picha: AP

Uhispania ndiye kinara wa kundi C ikiwa na pointi 7 ikifuatiwa na Italia yenye pointi 5. Croatia imefungasha virago ikwa na pointi 4 huku wanajamhuri wa Ireland wakitupwa nje ya mashindano hayo bila hata pointi moja. Kwenye mshikemshike wa robo fainali, Waspaniola watacheza na timu ya pili kutoka kundi D hapo siku ya Jumamosi kwenye dimba la Donetsk Ukraine. Waitaliano wao watakutana na kinara wa kundi D mjini Kiev siku ya Jumapili.

Ushindi haukupatikana kirahisi

Akiuelezea mchezo wa timu yake na Croatia kiungo wa kati wa Uhispania Andres Iniesta amesema kuwa mambo yalikuwa magumu. "Tulikuwa karibu kufuzu robo fainali, lakini pia karibu kuyaaga mashindano. Hatukutaka kuteseka namna hii, lakini sasa tunasonga mbele" alisema.

Andres Iniesta, wa timu ya taifa ya Uhispania
Andres Iniesta, wa timu ya taifa ya UhispaniaPicha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wake Kocha wa Italia Cesare Prandelli alisema mchezo baina ya timu yake na Ireland ulikuwa mgumu sana. "Tulikabiliana na timu ambayo ilitutesa. Leo tumejua kuwa pamoja na ubora wa timu pia, pia unahitaji sana moyo wa subira. Tumeweza kutengeneza nafasi nzuri za kushinda na nina matumini hali itakuwa hivyo kwenye mchezo ujao" alimaliza kusema.

Wakroatia walijiona wenye mikosi baada ya kukataliwa penalti na mwamuzi wa mchezo wake na Uhispania Mjerumani Wolfgang Stark kwenye dakika ya 27 kipindi cha awali kutokana na kucheza vibaya kwa Sergio Ramos dhidi ya Mario Mandzukic.

Kitimtim cha leo

Hii leo kutakuwa na kizaazaa kingine hapo timu za kundi D zitakapokamilisha michezo ya makundi nchini Ukraine. Sweden itacheza na vijana wa Francois Holande, Ufaransa kwenye dimba la Olympic Stadium wakati Uingereza itakwaana na wenyeji wenza wa mashindano hayo Ukraine kule dimbani Donbass Arena.

Mchuano uliopita kati ya Ukraine na Ufaransa
Mchuano uliopita kati ya Ukraine na UfaransaPicha: Getty Images

Kwa upande wangu ni hayo tu Dahman niliyokuwa nayo asubuhi hii kutoka kwenye fainali za mataifa hapa barani Ulaya yaani Uefa Euro 2012.

Mwandishi: Stumai George/DPAE