1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Mpox sio janga kama COVID-19

20 Agosti 2024

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema homa ya nyani, mpox sio janga jingine jipya kama ilivyokuwa COVID-19, kwa sababu maafisa wanafahamu vizuri kuhusu virusi hivyo na njia ya kujikinga na ugonjwa huo na kuzuia usienee.

https://p.dw.com/p/4jhhz
Mikono ya mtu mwenye ugonjwa wa mpox
Mikono ya mtu mwenye ugonjwa wa mpoxPicha: Brain WJ/BSIP/picture alliance

Mkurugenzi wa WHO, barani Ulaya, Hans Kluge amesema kuwa mpox sio ugonjwa mpya wa COVID na hatua za kuudhibiti zinaendelea kuchukuliwa.

''Tunajua jinsi ya kudhibiti mpox. Na barani Ulaya, tunajua hatua zinazohitajika kuzuia maambukizi yake kabisa. Miaka miwili iliyopita, tulidhibiti mpox barani Ulaya kutokana na ushirikiano wa moja kwa moja na jamii zilizoathirika zaidi za wanaume wanaoshiriki mapenzi na wanaume wenzao,'' alifafanua Kluge.

Kluge: Mpox kutosababisha kufungwa shughuli za maisha

Akizungumza Jumanne na waandishi habari mjini Geneva kwa njia ya video wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa, Kluge amesema mabadiliko ya tabia, hatua za afya ya umma zisizo na ubaguzi, na chanjo ya mpox ilichangia kudhibiti mripuko huo, hivyo hatari kwa watu kwa ujumla ilikuwa ndogo. Amesema WHO barani Ulaya haitotangaza kusitisha shughuli za maisha kama ilivyokuwa wakati wa janga la COVID-19.

Mkurugenzi wa WHO, barani Ulaya, Hans Kluge
Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Hans KlugePicha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa Kluge, takribani visa 100 vya kirusi kipya vinarekodiwa kwa mwezi barani Ulaya. Watalaamu wa afya wamesema aina mpya ya kirusi Clade 1b kinaonekana kuambukiza zaidi kuliko aina ya virusi iliyopita, na pia ina uwezakano mkubwa wa kusababisha maambukizo makali. Hata hivyo, Kluge amesisitiza kuwa hadi sasa kuna kisa kimoja tu cha Clade 1b  barani Ulaya, ambacho kimeripotiwa nchini Sweden.

WHO bado haijapendekeza matumizi ya barakoa

Aidha, msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema shirika hilo halipendekezi matumizi ya barakoa, wala chanjo ya watu wengi. Kulingana na Jasarevic, wanapendekeza matumizi ya chanjo katika mazingira ya mripuko kwa makundi ambayo yako katika hatari zaidi.

Agosti 14, WHO ilitangaza hali ya dharura ya afya ya umma kimataifa, kutokana na kuongezeka kwa visa vya aina mpya ya kirusi Clade 1b katika Jamhuri ya Kidemokarsi ya Kongo na kuenea kwake kwenye nchi jirani.

Kibao cha ofisi ya kampuni ya kutengeneza madawa ya Bavarian Nordic
Kibao cha ofisi ya kampuni ya kutengeneza madawa ya Bavarian Nordic Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Afrika, CDC Jean Kaseya, amesema mazungumzo tayari yameanza na kampuni ya madawa ya Denmark ya Bavarian Nordic kuhusu upelekaji wa teknolojia yake mpya ya chanjo za mpox, ili iweze kutengenezwa barani Afrika katika siku zijazo.

Kaseya ameyatoa matamshi hayo wakati akizungumza na waandishi habari siku ya Jumanne, na kwamba atatoa taarifa zaidi wakati wa mkutano wake na kampuni ya Bavarian Nordic katika wiki zijazo.

Naye mkurugenzi mkuu wa Bavarian Nordic, Paul Chaplin amesema kampuni hiyo inaweza kuongeza uzalishaji wa chanjo yake ya mpox hata kabla ya kupokea oda, lakini hilo litategemeana matokeo ya mkutano wake na WHO utakaofanyika wiki hii.

(AFP, DPA, Reuters)