Ugiriki yatapatapa hatima ya mfuko wa uokozi kujadiliwa
28 Septemba 2011Ifahamike kuwa Ugiriki inazongwa na madeni makubwa na nakisi ya bajeti. Yote hayo yanajiri baada ya Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin.
Uwekezaji na mikopo
Katika hotuba yake aliyoitoa mjini Berlin, Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou aliweka bayana kuwa nchi yake imejitahidi kuchukua hatua muhimu katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Akiwahutubia wafanyabiashara na wanasiasa Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou aliwasisitizia kuwa kuwekeza nchini mwake kuna manufaa kwani, "Tumefanya mageuzi ambayo hatukuyatarajia katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Ni kweli tatizo hili la kiuchumi linatupa fursa ya kuomba usaidizi. Hata hivyo, munapowekeza Ugiriki ndipo mutatusaidia kujikwamua. Hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kutupeleka pazuri katika siku za usoni.
Kudaiwa si ufukara
Ugiriki inayozongwa na madeni makubwa si nchi masikini. Kwa upande mwengine, wafanyabiashara katika sekta ya viwanda waliweka bayana kuwa haitowezekana kuwekeza nchini Ugiriki kwa sasa. Ifahamike kuwa endapo Ugiriki haitopewa mikopo na mfuko maalum ulioandaliwa wa kuyasaidia mataifa yanayokabiliwa na madeni, itafilisika. Hatma ya mfuko huo itaamuliwa hapo kesho hususan masuala ya uwezo wake na mfumo mzima wa kutoa mikopo. Kwa upande wake, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anasisitiza kuwa ipo haja ya kuisaidia Ugiriki.
"La msingi hapa ni, tunalazimika kwa upande wetu kutoa msaada unaohitajika kwa minajili ya kuisaidia Ugiriki iweze kujisimamia baadaye ili tuweze kuondoka katika kipindi hiki kigumu….na kuzizuwia taarifa mbaya kusambaa kila mwezi….matokeo ambayo yanayaathiri masoko kwa jumla. Dhamira yetu ni kuirejesha Ugiriki katika mkondo wa sawa."
Euro hatarini
Kwa upande mwengine, washirika wa sekta ya uchumi wana mtazamo tofauti na wanahisi kuwa sarafu ya euro iko hatarini.
Yote hayo yakiendelea, Bunge la Ujerumani, Bundestag, linatazamiwa kulipigia kura hapo kesho suala la kuuongeza uwezo wa mfuko huo wa uokozi pamoja na vigezo vya kutoa mikopo yenyewe. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou anafafanua kuwa hali yote kwa jumla inawavunja moyo Wagiriki wanaolazimika kubana matumizi kwa kiasi kikubwa, " Hii ndiyo sababu malalamiko yote ya kuikosoa Ugiriki yanatuvunja moyo kwa kweli….si tu katika uongozi ambao unajitahidi kwa kiasi kikubwa kuvitimiza vigezo vilivyowekwa wakati ambapo uchumi unazidi kudorora , bali pia kwa raia wa kawaida wanaojitahidi kupambana na hali halisi pamoja na mabadiliko makubwa."
Tathmini ya kiuchumi
Serikali ya Ugiriki inajitahidi kwa kila hali kuwarai wenzao wa mataifa ya bara la Ulaya ambao pia ni wafadhili wake, kwamba wanafanya mageuzi yaliyo na azma ya kuibadili hali pasina kujali athari za kisiasa. Wakati huohuo, ujumbe wa IMF, Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Umoja huo unatarajiwa kuelekea Athens hapo kesho kwa minajili ya kuikagua hali halisi ya kiuchumi ya Ugiriki.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-ZPR-Nina Werkhäuser
Mhariri:Miraji, Othman