Ugiriki yaikubali dawa chungu
14 Agosti 2015Wakati Mawaziri hao wakikutana mjini Brussels kuupitisha mpango wa euro bilioni 85 wa kuuokoa uchumi wa Ugiriki, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Alexis Tsipras ameonya mpango wowote wa Ujerujmani wa kuifanya nchi hiyo isipokee mkopo unaotarajiwa itakuwa ni pigo kubwa na kuirejesha nchi hiyo katika mgogoro usiomalizika.
Tsipras amewaomba wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya kukataa pendekezo lingine lililokuwa limependekezwa na Ujerumani, ambapo amesema pendelezo hilo litarefusha matatizo yaliopo. Ugiriki inahitaji kupata mkopo huo kabla ya muda wa mwisho wa kulipa deni lake la euro bilioni 3.4 kwa benki kuu ya ulaya kupita mnamo Agosti 20 mwezi huu.
Uwezekano wa uchaguzi wa mapema
Takriban wabunge 222 wameupigia kura mpango huo ulio na kurasa 400-huku wabunge 64 wakipiga kura ya kuupinga wakiwemo wabunge 40 kutoka chama cha mrengo wa shoto cha Syriza cha Waziri Mkuu Tsipras. Ni wabunge kumi na mmoja tu ambao hawakushiriki katika shughuli hiyo ya upigaji kura.
Tsipras ameungwa mkono na wabunge 118 kati ya 162 wa chama chake, kuhusu mkopo wa Euro bilioni 86 kutoka kwa wakopeshaji. Uungwaji mkono huo hata hivyo haukufikia idadi ya wabunge 120 wanaohitajika kupiga kura kuiwezesha Serikali ya wachache kuendelea kuwa madarakani.
Kwa upande wake aliyekuwa waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama cha Syriza walikataa kuunga mkono mpango huo wa miaka mitatu ambapo awali waziri huyo mkuu alisema hatua hiyo itamfanya aitishe uchaguzi wa mapema.
Tsipras amesema iwapo mpango huo utafeli kupitishwa basi utaifanya Ujerumani kupitisha pendekezo lake la kuwepo kwa mkopo wa dharura hadi pale watakaposawazisha masharti yote muhimu ili kupewa msaada kamili. Ujerumani inasisitiza Ugiriki itoe maelezo zaidi juu ya mpango wake kabla ya kuukubali.
Hata hivyo Tsipras ataendelea kuongoza Serikali hadi sehemu ya kwanza ya deni hili jipya itakapolipwa, hatua ambayo itamuezesha kuwasilisha Bungeni kura ya imani juu ya serikali yake. Duru zasema kuwa hayo yatafanyika mwezi huu huu wa agosti tarehe 20.
Muandishi: Ambia Hirsi/AFP/dpa
Mhariri: Gakuba Daniel