1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki imefilisika ?

28 Aprili 2010

Vipi kuiokoa na kuzuwia kupungua thamani ya euro ?

https://p.dw.com/p/N8aj
George Papaconstantinou-waziri wa fedha wa Ugiriki.Picha: AP

Kwa jicho la gharama kubwa za kuhudumia madeni yake, Ugiriki, imeungama binafsi kwamba, sasa haiwezi kukopeshwa tena kwenye masoko ya fedha.Shirika linalotathmini uwezo wa kukopa,limeiorodhesha Ugiriki kuwa nchi yenye madeni kope si zake. Kutothaminiwa Ugiriki kukiendelea zaidi nako, kunaushinikiza zaidi Umoja wa Ulaya kuamua haraka kuiokoa Ugiriki tena haraka kabla ya jahazi kuzama.

Ugiriki imefilisika. Baada ya dhamana zake za mikopo ilitoa kuwa si chochote si lolote,mwanachama huyu wa Umoja wa Ulaya, hawezi tena kukopa katika masoko ya fedha kwa masharti yanayovumilika. Endapo Mei 19, Ugiriki haitamudu kulipa deni lake la Euro bilioni 8.5 linalobidi kulipwa siku hiyo,Ugiriki itajikuta pangu pakavu.Hapo,Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Umoja wa Ulaya ,litabidi kujiingiza kati kuiokoa Ugiriki na yakitaka au yasitake, hayana njia nyengine. Kusita-sita kwa Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, hapo kutakoma.Hali ya kutoafikiana iliopo kati ya mawaziri wa serikali yake na wabunge juu ya swali la kuiokoa Ugiriki,kumechangia pia kuiangusha zaidi Ugiriki.

Wawekezaji wana shaka shaka iwapo na lini Umoja wa ulaya kweli utaiokoa Ugiriki kwa mikopo. Kwani, mambo yanakwenda haraka sana.Shirika la kutathmini uwezo wa nchi kukopeshwa(Standard & poor's ) limeshaipitishia Ugiriki, adhabu ya kifo. Na nguzo nyengine tayari inatikisika. Ureno nayo, imeshapoteza uaminifu wake wa kustahiki kukopeshwa.Madeni makubwa yanaitikisa nchi hii. Mpango wa hadi sasa wa kubana matumizi,unaangaliwa hautoshi kutibu maradhi. Masoko yasiojitaja ya fedha yalioikopesha Ureno, mabilioni ya fedha, nayo sasa yameanza kulenga mizuinga yao upande wa Ureno.

Na ikiwa Umoja wa Ulaya, kwa muda wa siku chache tu ,hautajitokeza kumnusuru mwanachama wake ,basi hata Ureno nayo, itatumbukia shimoni.

Wiki hii inapaswa mkutano maalumu wa kilele wa marais na viongozi wa serikali za Umoja wa ulaya ufanyike ili kuyaonesha masoko kwamba hawaruhusu mchezo mbaya na usioruhusiwa unaochezwa na watiaji-raslimali,pepo za wakwepaji-kodi na wengineo kuchafua mambo.Umoja wa ulaya usiachie tena kuburuzwa na masoko ya fedha bali binafsi uchukue hatua kudhibiti hali ya mambo.

Njia mojawapo ya kuiokoa Ugiriki na Ureno , ni kwa Umoja wa Ulaya na Banki kuu ya Ulaya,kununua dhamana za mikopo za serikali za Ugiriki na Ureno, ili kuzima uvumi na dharuba inazozipiga nchi hizo 2.Ingawa hii hairuhusiwi kwa muujibu wa Mkataba wa UU,lakini hali hii iliozuka sasa ,waasisi wa sarafu ya Umoja wa Ulaya (Euro) , hawakuitazamia miaka 15 iliopita.Mikataba inaweza kubadilishwa na hata kurekebishwa.Umoja wa Ulaya, ni Jumuiya yenye hatima moja na hivyo , isiachiwe kusambaratika.

Mwandishi: Riegert,Bernd/ DW-ZPPR -europa

Mtayarishi: Ramadhan Ali:

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman