Ughali wa maisha wafikia asilimia milioni 1 Venezuela
26 Julai 2018Mapema wiki hii , shirika la fedha la kimataifa IMF limetoa viwango vinavyotisha, likifanya marekebisho kwa makadirio yake kwamba ughali wa maisha utafikia asilimia 14,000 katika idadi ambayo imeongezeka kwa karibu mara 70. Tayari, umasikini unafikia viwango ambavyo havivumiliki, watu wanaokadiriwa kufikia milioni 1.6 wameikimbia nchi hiyo , vurugu za kijamii zinaongezeka miongoni mwa wale waliobakia, mishahara imekuwa karibu haina thamani tena, kuna upungufu wa chakula na madawa, na bado rais Nicolas Maduro anaendelea kung'ang'ania madarakani.
"Hakuna kitu kinachonishangaza," Marcos Salazar aliliambia shirika la habari la afp baada ya kuambiwa kuhusu makadirio hayo ya IMF wakati akila mkate huku akiwa amesimama katika kioski mtaani.
Mkate huo na nyama unagharimu kiasi cha boliva milioni tano sarafu ya Venezuela kiasi ya dola 1.5 katika soko la chini kwa chini , ikiwa na thamani ya mshahara wa mwezi mmoja, ambao unalipwa kwa kutumia vocha za chakula.
Kila wiki , kila siku , vitu vinaongezeka bei. Sio kwa taratibu , bei zinalipuka," aliongeza Salazar , profesa mwenye umri wa miaka 31 anayefanyakazi tatu, ambazo bado hazitoshi kuweza kumfanya amudu maisha yeye pamoja na mpenzi wake.
Wanaishi kutokana na pesa zinazotumwa na ndugu ambao wamekimbia nchi hiyo.
Ughali huo mkubwa wa maisha sio tu umechangia katika upungufu wa chakula na madawa lakini pia kuporomoka kwa huduma za umma , ikiwa ni pamoja na maji, umeme na usafiri.
Mageuzi ya kisiasa
Mtaalamu Henkel Garcia wa washauri wa kiuchumi , Econometrica, anaamini Venezuela inahitaji kwa udi na uvumba mageuzi ya kisiasa na kijamii ili kuweza kufanikisha uthabiti wa wastani.
"Unaweza tu kukimbia kutoka katika ughali huu mkubwa wa maisha kupitia mageuzi makubwa ya sera za kiuchumi," aliliambia shirika la habari la afp, akielekeza katika mifano ya Ujerumani katika miaka ya 1920 na Zimbabwe katika miaka ya 2000.
Umasikini umepanda hadi asilimia 87 katika mwaka 2017 na umasikini wa kupindukia umefikia asilimia 61 , kwa mujibu wa kundi la vyuo vikuu vya Venezuela.
Kundi hilo limesema sita kati ya watu 10 wanadai wapoteza wastani wa kilo 11 kutokana na njaa. Serikali ya Maduro inakataa tarakimu hizo , ikidai kwamba umasikini uliokithiri uko katika asilimia 4.4 tu.
Venezuela, hata hivyo , inategemea mauzo ya mafuta ambayo yanafanya kiasi ya asilimia 96 ya mapato , lakini uzalishaji umepungua na kuwa katika kiwango cha chini kabisa katika muda wa miaka 30, mapipa milioni 1.5 kwa siku, kutoka mapipa milioni 3.2 mwaka 2008, kwa mujibu wa shirika la mataifa yanayosafirisha kwa wingi mafuta.
Hali hii imeizuwia nchi hiyo kufaidika na kupanda kwa bei ya mafuta, wakati uamuzi wa serikali ya rais Maduro kuchapisha fedha kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni umesababisha kudhoofika kwa uchumi.
Shirika la IMF likihalalisha makadiro yake lilisema linatarajia serikali kuendelea kuchapisha noti zaidi , na kutia nguvu kasi ya ughali wa maisha wakati mahitaji ya fedha yakizidi kuporomoka."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusuf, Saumu