Mwanahabari Moses Mbayo aachiliwa kwa dhamana
6 Machi 2020Kesi ya Moses Bwayo, mwanahabari aliyekamatwa mwezi uliopita imesikilizwa leo Ijumaa mjini Kampala . Bwana huyo na wenzake walikuwa wakitekeleza kandarasi waliopewa na kampuni moja ya Uingereza kutengeneza video ya muziki ya msanii na mwanasiasa Robert Kyagulanyi - maarufu Bobi Wine. Hata hivyo washtakiwa hao wameshangaa baada ya kusomewa mashtaka tofauti na waliosomewa awali.
Mawakili wao wanasema kesi hiyo imegeuzwa kuwa ya kisiasa kwani ni tofauti kabisa na ile waliosomewa hapo awali ya kutatiza shughuli za watumiaji wa barabara.
Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa hao tisa wamepewa dhamana ya shilingi laki tatu pesa taslimu za Uganda huku wadhamini wao wakitakiwa kusaini dhamana ya shilingi milioni tano.
Tangu alipotangaza kuwania urais, Bobi Wine amekabiliwa na wakati mgumu katika harakati zake za kushauriana na wananchi kuhusu mikakati yake. Lakini shughuli kama hiyo ya kurekodi video ni mojawapo ya njia za kuingiza kipato kwa msanii huyo. Asasi mbalimbali za kupigania haki za wanahabari zimekosoa utawala wa Uganda kwa kumzuia mwandishihabari Moses Bwayo kufanya kazi yake. Washtakiwa watafika tena mbele ya hakimu tarehe 15 mwezi Aprili.