1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ufaransa yamaliza shughuli ya kuwaondoa wanajeshi wake Niger

23 Desemba 2023

Ufaransa imekamilisha shughuli ya kuwaondoa wanajeshi wake nchini Niger baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mamlaka ya kijeshi nchini humo

https://p.dw.com/p/4aWRx
Wanajeshi wa Ufaransa katika ukanda wa Sahel waliokamilisha ziara ya kikazi ya miezi minne katika eneo la Sahel waondoka katika kambi yao ya Gao nchini Mali mnamo Juni 9, 2021
Wanajeshi wa Ufaransa katika ukanda wa SahelPicha: AP Photo/picture alliance

Hatua ya Ufaransa ya kuondoa wanajeshi wake nchini Niger inakamilisha miaka kadhaa ya msaada wa kijeshi na kuzua wasiwasi miongoni mwa wachambuzi kuhusu ombwe katika vita dhidi ya vurugu za makundi ya itikadi kali katika eneo la Sahel.

Soma pia:Ufaransa yawaondoa wanajeshi wake wa mwisho Niger

Mkuu wa jeshi la Ufaransa, ameliambia shirika la habari la AP kupitia barua pepe kwamba ndege ya mwisho ya jeshi hilo iliyowabeba wanajeshi wake, iliondoka Niger hapo jana ikiwa ni siku ya mwisho iliyowekwa na utawala huo wa kijeshi uliokata uhusiano na Ufaransa baada ya mapinduzi ya mwezi Julai. 

Soma pia:Kundi la mwisho la kikosi cha Ufaransa kuondoka Niger leo

Ufaransa tayari ilitangaza wiki hii kwamba itafunga ubalozi wake nchini Niger kwa "muda usiojulikana."

Hata hivyo wakati wa ziara yake nchini Jordan siku ya Alhamisi, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema nchi yake itaendelea kuhusika katika eneo la Sahel ambalo limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya makundi ya itikadi kali.

Utawala wa kijeshi wa Niger, umetaja kukamilika kwa ushirikiano huo wa kijeshi na Ufaransa kuwa mwanzo wa ''enzi mpya'' kwa raia wa nchi hiyo.